Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akimsikiliza mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya Meli ya
Skagit, Kitwana Makame Ali (24) mkazi wa Unguja, wakati alipotembelea
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, leo Julai 19, 2012
kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo baada ya kuokolewa
katika ajali hiyo iliyotokea jana eneo la Kisiwa cha Chumbe. Kulia ni
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia
Suluhu Hassan.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akimsikiliza mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya
Meli ya Skagit, Masembe Enos (32), mkazi wa jijini Mwanza aliyekuwa
akisafiri na mkewe ambaye mpaka sasa hajapatikana.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na mgonjwa aliyenusulika katika ajali ya Meli ya
Skagit, Hamisa Akida (45) mkazi wa Ununio mjini Bagamoyo, wakati
alipotembelea katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya
Meli ya Skagit, Stephano Lufyagila (22), mkazi wa Kiwalani jijini Dar es
Salaam.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na vijana wawili, Hans Manoni (kulia) na Nsunga
Joseph, waliokuwa wakisafiri na wenzao wawili ambao wamefariki katika
ajali hiyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akimsalimia Salome Abeid Mwambaga (33) mkazi wa jijini Arusha,
mfanyakazi wa Kampuni ya Atomic Enegy Commissioner, aliyekuwa akisafiri
kuelekea Pemba kikazi ambaye pia amepoteza vifaa vya kazi na Document
zake zote muhimu katika ajali hiyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika Ikulu mjini
Zanzibar leo kwa ajili ya kumpa pole kuhusu ajali ya Meli ya Skagit
mali ya Kampuni ya seagull, iliyotokea jana eneo la Kisiwa cha Chumbe.
Wananchi wakiwa wamepanga foleni kuelekea kutambua miili ya marehemu katika Viwanja vya Maisara leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujionea shughuli hizo
katika viwanja vya Maisara mjini Unguja leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akijumjuika na wananchi katika moja ya familia iliyopotelewa na ndugu
katika ajali hiyo, mjini Zanzibar leo mchana.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika Ikulu mjini
Zanzibar leo Julai 19, 2012 kwa ajili ya kumpa pole kuhusu ajali ya
Meli ya Skiget mali ya Kampuni ya seagull, iliyotokea jana eneo la
Kisiwa cha Chumbe.
19/07/2012
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imebandika orodha ya majina ya wasafiri 340
waliokuwa katika meli ya Mv Skagit huku wananchi wakitakiwa kukuhakiki kama ndugu zao walikuwemo.
Aidha, Polisi jijini Dar es Salaam inamshikilia
Meneja wa meli hiyo, Omar Hassan Mkamnhongt (50) mkazi wa Magomeni ambaye ni
mmiliki wa Kampuni ya Seagul Transport Tawi la Dar es Salaam inayomiliki meli hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck amesema Polisi Kanda Maalumu inafanya
uchunguzi wa ajali hiyo, wakishirikiana na wadau mbalimbali kusaidia utambuzi
wa waliokufa, majeruhi wa Tanzania bara na wa Zanzibar pamoja na watalii kutoka
nje.
Akizungumza na baadhi ya wanandugu waliofika ofisini kwake, Sadiki amesema,
licha ya kubandika orodha hiyo, ofisi yake haina uhakika na idadi hiyo kwani
huenda walikuwepo zaidi ya hao. Alisema orodha ya majina hayo itabandikwa
katika ofisi yake na kwamba kila mwanandugu anayehitaji kufahamu zaidi
anatakiwa kufika na kutambua majina hayo.
Alisema ofisi yake pia inajaribu kuzungumza na wamiliki wa meli au boti
wasaidie wanandugu wanaotaka kwenda Zanzibar kutambua ndugu zao waliofikwa na
mauti kwenye ajali hiyo, “Wapo wanandugu hapa ambao wana uwezo na wanataka
kwenda Zanzibar ili kuwatambua ndugu zao, lakini wameshindwa kwenda kutokana na
meli nyingine kusitisha safari hivyo hao tunakwenda nao bandarini sasa hivi
(jana) ili kuwasaidia waweze kufanikisha safari yao,” alisema na
kuongeza: “Kwa wale ambao hawawezi kwenda leo (jana) tutahakikisha
tunafanya utaratibu ili kesho waweze kwenda kwa ajili ya kutambua maiti.
Kuhusu usalama wa meli hiyo, Sadiki alisema kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi wa
meli hiyo, inaonesha kwamba ilikaguliwa Agosti 24 mwaka jana na kwamba ilikuwa
inamalizika muda wake Agosti 23, mwaka huu, “Si kweli kwamba meli ilikuwa
haijafanyiwa uchunguzi… polisi wanafuatilia zaidi… na kuanzia leo (jana)
tunatengeneza fomu maalumu yenye jina la aliyepotea na anayetaka kwenda
Zanzibar kutambua maiti ambapo ataandikisha jina lake kwa Edward Mbanga aliyeko
katika ofisi za Mkuu wa Mkoa,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisema juzi walituma kundi kubwa la watu kwa ajili ya kusaidia shughuli ya
kuokoa.
Kova aliwataka ndugu na jamaa wa watu wanaohofiwa kufa katika meli hiyo,
waorodheshe majina ya ndugu zao, nguo walizokuwa wamevalia ili kikosi chake kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra)
walioko eneo la ajali, wasaidie kuwatambua.
19/07/2012
Juzi alipozungumza katika kipindi
cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV na kuongozwa na
Mtangazaji wa ITV, Selaman Semeyu, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alizungumzia pamoja na mambo mengine, fedha za mkopo,
Dola za Marekani milioni 20 zilizokuwa zimetolewa na Serikali ya Libya enzi za
utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hayati Muamar Gaddafi.
Pia aligusia upotevu wa Sh bilioni tatu katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Akizungumzia fedha hizo, Membe alisema baada ya Serikali ya Libya kuikopesha Serikali ya Tanzania kiasi
hicho cha fedha, baadaye Serikali za nchi hizo mbili zilikutana na kukubaliana
fedha hizo zikopeshwe kwa kampuni yoyote itakayozihitaji.
“Baadaye Serikali ya Libya
na Tanzania
zilikutana na kukubaliana fedha hizo zikopeshwe kwa kampuni yoyote itakayotaka
kukopa izikope na makubaliano haya yako kwenye maandishi. Baadaye ikaja
kampuni moja ya Meize kwa ajili ya kujenga kiwanda cha saruji kule Lindi na
wakati wa kampeni tukawaahidi wananchi wa Lindi kwamba kiwanda hicho
kitajengwa. Wakati tunaahidi hivyo, kumbe Kampuni ya Mohamed Enterprises
ilikuwa inashirikiana na ofisa mmoja wa ubalozi wa Libya apate fedha hizo na hapo
ukawa ugomvi.
“Pamoja na hayo, mimi nilisimamia kuhakikisha kiwanda hicho cha saruji
kinajengwa Lindi kama sehemu ya kumbukumbu
yangu. Lakini baadaye wananume wakabadilisha lugha, wakasema nimewapa marafiki
zangu, jamani fedha hizi ni makubalino ya nchi mbili na mimi ni ‘share holder’.
“Sasa nakwambia fedha hizi ziko TIB, nendeni kwa meneja wa TIB mumuulize, huu
ujinga gani huu unaozungumzwa, kwanza hata hizo Dola milioni 20 hazitoshi
kujenga kiwanda bali zinatakiwa Dola milioni 60.
“Sasa nataka niwaambie wananchi wa Lindi kwamba kiwanda cha saruji kitajengwa
Lindi, hivi vituko vinavyotokea nitavigonga vyote na ipo siku nitawaanika wote,
lazima watu hao wajue kwamba ukikaa juu ya nyoka, ipo siku atakugonga
tu. Hili nawaachia Watanzania waamue lakini kuna watu 11 wakiwamo
waandishi wawili wa habari, nitawatwanga kweupe, nyie suala la urais
2015 subirini tu nitawaanika peupe bungeni tena kwa majina,” alisema
Waziri Membe.
Suala la urais 2015
Alipoulizwa kama atagombea urais mwaka 2015, alishindwa kuweka wazi msimamo
wake kwa kile alichosema kuwa hajaoteshwa juu ya nafasi hiyo.
“Ole wao nioteshwe, ipo siku nitaoteshwa, najua nchi hii ina watu wanaoivuruga
na hawataki kuona mafanikio, ukisema unataka kujivua gamba utaona wana uwezo wa
kuchonga uongo, hao wanatumia vyombo vya habari kuchonga uongo. “Kwa
mfano, unawakaribisha vijana kama wa Chadema
nyumbani kwako unawapa chakula baadaye wanageuza mambo, we waache tu.
“Siku moja nitawatoa kwenye magazeti kila mmoja dozi yake, nitakuja kuwatandika
kila mmoja na kinachoniudhi ni kwamba hao watu wako ‘smart’ wana fedha na
wanataka kutawala hata kama hawana madaraka.
Ukiona mtu anaanza kudharau wakati hana madaraka, ujue hapo kuna
tatizo. “Jambo jingine ni kwamba ukianza kuona katika jamii kila tatizo
inalaumiwa Serikali, ujue kuna tatizo, ujue hapa kazi ipo.
Uchaguzi ndani ya CCM
Kuhusu uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema chama
hicho kina nafasi ya kujiimarisha kupitia uchaguzi huo. Alisema ana hamu
ya kufika mwaka 2015 ashuhudie uchaguzi mkuu utakavyokuwa.
“Nina hamu ya kufika mwaka 2015 nione akina nani watarudi maana kuna wabunge
wengine ni mahodari wa kuzungumza bungeni lakini majimboni
hawaendi. “Utakuta mbunge mwingine anasema haungi mkono bajeti, lakini
baada ya siku mbili anamuomba Waziri aliyepinga bajeti yake kwamba naomba fedha
za kupeleka jimboni kwangu. “Upinzani siyo kukataa bajeti, huwezi kukataa
bajeti yangu halafu kesho unakuja kuniomba fedha upeleke jimboni kwako,”
alisema.
Alitaka Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naye awe anaulizwa maswali
ya papo kwa papo kupima uwezo wake katika utendaji.
Maoni ya wabunge
Wakizungumza juu ya kauli za waziri huyo, baadhi ya wabunge wameonyesha
kutoridhishwa kutokana na nafasi aliyonayo katika Serikali.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alisema kitendo cha Membe kusema kuna
watu 11 wanaiyumbisha Serikali, hakitakiwi kufumbiwa macho kwa kuwa kinagusa
mamilioni ya Watanzania, “Huyu Membe aache maneno, hivi majuzi alisema
kuna watu anawafahamu wanahusika na mauzo ya rada, sasa anakuja na suala
jingine la watu 11 wanaoyumbisha nchi. “Kama
kweli anawajua kwa nini asiwataje, yaani wananchi wanataabika halafu yeye
anatwambia atawataja, mimi simuelewi, mwambieni awataje,” alisema Mpina.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (CHADEMA), alisema Membe anatafuta umaarufu
wa siasa kwa kuwa ana kitu anachokitaka, “Huyu tumemzoea, alisema hivi
karibuni kwamba anawajua wahusika wa rushwa ya rada na hadi sasa hawajawataja,
sasa unafikiri anataka nini. “Kama kweli hao watu wapo kwa nini asiwataje,
atutajie majina, lakini kama anadhani kuna watu kama
akina Lowassa wanataka kumkwamisha asigombee urais mwaka 2015, anajidanganya
kwa sababu yeye hawezi kupambana na Lowassa, huyo ni mtu mdogo kwa Lowassa,”
alisema Wenje.
Naye Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alionyesha kutoridhishwa na kauli ya
Membe na kusema kuwa hakumuelewa baada ya kutotaja majina ya watu hao 11.
“Mimi nilimuona akizingumza na nilipomsikia hivyo, nikashindwa kumuelewa kwa
sababu kama alichokuwa akikisema hakiendani na
madaraka yake. “Sasa kama kweli anawajua watu hao 11 kwa nini asiwataje,
atutajie kuwafanya wananchi waendelee kuiamini Serikali yao,” alisema Azzan.
Wakati
uchunguzi wa kimataifa ungali ukiendelea, gazeti la Raia Mwema limethibitishiwa
kuwa Rais mstaafu aliyepata kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na
mmoja wa kigogo wa juu wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wanahusika.
Mtandao huo wa kiongozi huyo mstaafu ambaye anazo ndoto za kuwania urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mwenzake ndani ya Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, wamefanya mpango huo na aliyepata kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia amepata kuwa mbunge wa
moja ya majimbo ya uchaguzi mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, tayari vyombo vya kimataifa vinaelekea
kukamilisha uchunguzi wake na kwamba, majina ya wahusika hao yatawasilishwa
serikalini kwa hatua zaidi.
Kwa ushirikiano maalumu, viongozi hao wanadaiwa kufanikisha meli za Iran kusajiliwa na kisha kupeperusha bendera ya Tanzania kwa
lengo la kukwepa vikwazo vya kimataifa vilivyoweka kupitia Umoja wa Mataifa
(UN).
Vigogo hao wanadaiwa kufanikisha mpango wao kupitia kwa kampuni ya Philtex ya Dubai, inayodaiwa kusajili meli za mafuta za Iran ili kupeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kukwepa vikwazo vya
kiuchumi iliyowekewa nchi ya Iran.
Katika toleo lake namba 248, gazeti hili liliripoti kuwapo kwa taarifa
kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa zikibainisha kuwa,
baadhi ya viongozi Zanzibar wamekuwa na maslahi
katika masuala ya usajili wa meli hizo za kimataifa jijini Dubai.
Katika habari hiyo kwenye gazeti hili, mwandishi wetu alinukuu moja ya chanzo
chetu cha habari akisema; “Unajua kuna hali ya kuzidiana ujanja, awali huku
Zanzibar walikataa SUMATRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Maji na Nchi
Kavu) kufanya shughuli zake na wakaunda Wakala wa Meli Zanzibar (ZMA) lakini
wakala huyu akatoa zabuni ya kusajili meli kwa kampuni iliyoko Dubai
(Philtex),”
“Baadhi ya viongozi hapa Zanzibar hawakujua ujanja uliopangwa na wenzao, ujanja
wa kuikataa SUMATRA Zanzibar na kuanzisha ZMA lakini pia ujanja wa kutoa zabuni
kwa kampuni ya Philtex ya Dubai. Sasa hivi ndiyo wanashituka kwamba wapo wenzao
wanaodaiwa kuhusishwa na kampuni hiyo,” kilieleza chanzo chetu cha habari
kutoka Serikali ya Zanzibar.
SIKU chache baada ya kusimamishwa
kazi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO), William Mhando na
wenzake: Robert Shemhilu, Lusekelo Kassanga na Haruna Mattambo, akaunti ya
mmoja wa vigogo wa shirika hilo
ngazi ya menejimenti iliyoko katika moja ya benki nchini imezuiwa na vyombo vya
dola nchini, Raia Mwema, limeelezwa.
Akaunti ya kigogo huyo (jina la benki na la mwenye akaunti yanahifadhiwa ili
kutoharibu uchunguzi unaoendelea) imekutwa na fedha zaidi ya shilingi bilioni
moja na sasa inadaiwa kuzuiwa kwa baraka za mamlaka za juu.
Vyanzo kadhaa vya habari vimeeleza ya kuwa kigogo huyo amekutwa na mabilioni
hayo ya fedha huku chanzo cha mapato hayo yasiyolingana na kipato chake kama mtumishi wa umma kikiwa ni utata.
Hata hivyo, wakati uchunguzi huo wa awali unaofanywa na vyombo vya dola nchini
ukiwa unaendelea, kwa upande mwingine kumebainika kuwapo na kampeni kali za kuuokoa
uongozi wa TANESCO unaochunguzwa kwa sasa, juhudi ambazo zimekuwa zikihusisha
hata Kamati za Bunge.
Kamati za Bunge ambazo baadhi ya wajumbe wake wanahusishwa katika ‘kuokoa’
jahazi la uongozi wa TANESCO uliosimamishwa ni pamoja na Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo sasa wanatajwa kuanza kumwandama Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi pamoja na Waziri Profesa Sospeter
Muhongo na Naibu wake, George Simbachawene, wanaotajwa kuwa na msimamo mkali
dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe na ubadhirifu ndani ya TANESCO.
Mgawo feki wa umeme
Hujuma kwa mtambo wa Kinyerezi
Wabunge watajwa
Alhamisi, Julai 19, 2012
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya ajali
ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea jana, Jumatano, tarehe
18, Julai 2012 katika eneo la Chumbe, Zanzibar.
Kutokana na msiba huu mkubwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa Taarifa kwa
Wananchi kuwa imesitisha Mikutano ya kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba
Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba. Mikutano iliyositishwa
ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia leo, Alhamisi, Julai 19, 2012 hadi
Jumamosi, Julai 21, 2012 katika maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri,
Pujini, Gombani na Wara.
Zoezi la kukusanya Maoni litaendelea kuanzia Jumapili tarehe 22,
Julai, 2012. Ratiba ya Mikutano katika maeneo yaliyositishwa
itatolewa baadaye.
Tume ya Mabadilikio ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa mabadiliko
haya hayahusu mikutano ya kukusanya maoni inayoendelea kufanyika katika mikoa
sita (6) ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera na
Manyara. Tume inawaomba wananchi wa Mikoa hii kujitokeza kwa wingi
na kutoa maoni yao.
Mwisho, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa pole kwa wafiwa, majeruhi na wote
walioguswa na ajali hii na tunamuomba Mwenye Mungu azilaze roho za marehemu
mahali pema peponi na majeruhi wote wapone kwa haraka.
Imetolewa na:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM,
Simu: 2137833,
Simu ya Mkononi: 0757 500800