Thursday, July 5, 2012

SOKO LA SIDO MWANJELWA LAFUNGWA BAADA YA KIBANDA KIMOJA CHA MAMA NTILIE KUNUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO. MAMA NTILIE MBIONI KUFUNGULIWA MASHTAKA - MBEYA.

Sehemu ya Soko la Sido Mwanjelwa lililoteketea kwa moto Jijini Mbeya,mnamo Septemba 16 mwaka jana na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
*****
Na  Venance Matinya, Mbeya.
Halmashauri ya Jiji la Mbeya inatarajia kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wa soko la Sido Mwanjelwa kutokana na kuhusishwa na vyanzo vya moto katika soko hilo mara kwa mara.
 
Baadhi ya wafanyabiashara hao ni wale wanaoshughulika na huduma za kupika na kuuza vyakula ndani ya soko hilo ambapo imedaiwa kuwepo na makubaliano kati ya viongozi na wafanyabiashara wa soko kutoruhusiwa kuwasha mkaa,sigala au moto na kutopika kitu chochote sokoni hapo.
 
Uongozi wa Jiji umesema watuhumiwa hao wamekiuka makubaliano na sheria ndogo ndogo zinazohusu soko hilo ambazo ni kifungu cha 12(1) cha mwaka 2011 ambacho kinakataza kujihusisha au kuwasha moto ndani ya soko hilo ili kuepuka majanga hayo.
 
Makamu Mwenyekiti wa soko la sido Bwana Wilson  Mwakisilwa alisema majanga hayo yamekuwa yakiliandama soko hilo tangu mwaka juzi ambapo wafanyabiashara wengi walipoteza mali zao na kusababisha waendelee kudaiwa kutoka katika taasisi za fedha.
 
Alisema hali hiyo inatosha na ndiyo sababu wameamua kuwafikisha mahakamani wale wote ambao wanakiuka makubaliano na kuendelea kusababisha hali ya hatari katika masoko na kusababisha wananchi kushindwa kufanya biashara zao kwa uhuru.
 
Mwakisilwa alisema wamefikia uamuzi huo baada ya juzi baadhi ya mama ntilie kuwasha moto na kusababisha kubanda kimoja kunusurika kuungua hali iliyosababisha taflani kubwa sokoni hapo na kuleta malumbano kati ya uongozi wa soko na wafanyabiashara.
 
“ Juzi jioni mama mmoja alikuwa akipika ndani ya kibanda na kusababisha moto kuwaka ingawa tulifanikiwa kuuzima lakini hawa akina mama  hawakuwa na lugha nzuri kwetu sisi na kusababisha tukose maelewano hali iliyotulazimu kwenda kwenye vyombo vya dola na hapa tumewakamata watu 9 waliohusika na hali hiyo” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
 
Aidha makamu mwenyekiti huyo aliwataja watu hao watakaofikishwa mahakamani kuwa ni Halima Benard, Lukia Kayuni, Maria Mwakamela,Elizabeth Sikwesi, Agnes Dominick, Rehema Musa, Beth Aron, Agatha Hussein na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Skauti.
 
Kwa upande wake baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo Michael Ashibaye na Lucia Silingwa waliwalalamikia mama ntilie kwa kutokuwa na uchungu wa mali wanazounguliwa hivyo kufikia hatua za kukaidi maagizo wanayokubaliana nayo.
 
Kamanda wa polisi wa wilaya ya Mbeya (OCD) Abraham Silvester alisema Uongozi wa Jiji wako tayari kuandaa hati ya mashtaka tayari kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao ambapo aliongeza kuwa watuhumiwa wote wanashikiriwa katika kituo cha kati cha polisi.

KAMPUNI ya simu za mkononi Zanzíbar ZANTEL kudhamini tuzo za wanamuziki bora Zanzibar

Na Ali Issa   Maelezo Zanzíbar    
                                                        
KAMPUNI ya simu za mkononi Zanzíbar ZANTEL imeahidi udhamini wa Shl. milioni 32 pesa taslimu kwa Kampuni ya Zanzibar Medium Corporación  kwa ajili ya tunzo ya wana muziki bora wa Zanzíbar mwaka 2012.

Udhamini huo umetangazwa leo na Mkurugenzi wa Biashara Zantel upande wa Zanzibar Mohammed Mussa wakati akizungumza na wandishi wa habarí katika ukumbi wa Idara ya Habarí Maelezo mjini Zanzíbar.

Amesema pesa hizo zimetolewa kwa ajili ya kudhamini tunzo hiyo ikiwa ni njia moja wapo ya kuthamini na kuheshimu mchango ambao wanamuziki wa Zanzíbar wamekuwa wakiutoa ikiwa ni pamoja na kuielimisha na kuiburudisha jamii. 

Ameongeza kuwa Kampuni ya kizalendo ya Zantel imekuwa ikitoa huduma zake na kujenga mapenzi ya dhati kwa jamii ikiwemo kujenga visima vya maji sita ili kuhakikisha faida inayopatikana inaifaidisha jamii kwa ujumla

Mkurugenzi huyo alisema pesa hizo zitatolewa kwa kuzingatia misingi imara na kuepuka upendeleo na kwamba Zanzitel itaendelea kuwa karibú na jamii kwa kutoa ushirikiano pale ambapo itahitajika.

Kwa upande wake Meneja Masoko kutoka Kampuni ya Zanzibar Medium Corporación ambao ndio waandaaji wa tunzo hiyo Said Khamis aliishukuru kampuni ya Zantel kwa kudhamini tunzo hizo na kuiomba indelee kuwa karibú na jamii pale ambapo watahitajika kutoa msaada wao.

Aidha amefahamisha kuwa tunzo hizo ambazo zitatolewa zitakuwa zimegawika katika makundi 16  ya aina mbali mbali za wasanii ikiwemo makundi ya muziki wa kizazi kipya (Zenji Fleva) na Taarab asilia.

Tamasha hilo la saba litafanyika Bwawani siku ya Ijumaa,Juni 6 mwaka huu ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa  Tanzania Dk.Mohammed Gharib Bilali .

No comments:

Post a Comment