Friday, February 24, 2012


Ziara ya Mbunge wa njombe Magharibi zawafurahisha wananchi wa jimbo lake.

Naibu waziri wa maji ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Njombe Magharibi Mhandisi Gerson Lwenge ameanza ziara ya siku nane kuwatembelea wananchi wa jimbo lake huku akieleza mambo mbalimbali pamoja na kuchangia maafa yanayo likumba jimbo hilo.

Katika ziara hiyo jana  Waziri Lwenge ameanzia katika  kata ya Igima kwa kuanza na kitongoji cha mawindi ambako ametoa  shilingi laki tatu ili kuanzishia mfuko wa maafa ya kijiji ikiwa ni zoezi la kuanzisha mifuko hiyo kwa kila kijiji jimboni humo.

Jumla ya nyumba Tatu zilikumbwa na maafa hayo kufuatia kunyesha kwa mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali februari 11 mwaka huu  na kusababisha hasara kubwa katika nyumba hizo zinazogharimu takribani milioni mbili ukarabati wake.

Akisoma taarifa ya kijiji cha Igima mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Igima mwl.Cremence Mwalongo amesema  kuwa licha ya mafanikio mbalimbali yaliyopo kijijini hapo lakini pia kijiji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kielimu.

Baadhi ya changamoto zilizobainishwa kwenye Risala hiyo ni pamoja na ukosefu wa vifaa mbalimbali katika shule ya sekondari ya Igima hali iliyopelekea shule hiyo kushindwa kufanikisha hata mwanafunzi mmoja kujiunga na kidato cha tano mwaka huu kati ya wanafunzi 121.

Kufuatia changamoto hizo pia mhandisi Lwenge hakusiti kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa kijiji hicho kuachana na itikadi za kisiasa kwa kipindi hiki badala ya kujikita katika shughuli za kimaendeleo.


Ziara hiyo kwa siku ya leo inaendele katika kata ya Ulembwe ikianzia kijiji cha Ulembwe huku ikimalizika katika kijiji cha Usalule ukiwa ni muendelezo wa ziara yake ya juma zima.

No comments:

Post a Comment