Monday, May 14, 2012

Mbunge amshauri Kigoda kunusuru viwanda 

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemshauri Waziri  wa Viwanda, Biashara  na Masoko, Dk Abdallah Kigoda, kuweka kipaumbele katika kunusuru viwanda vilivyoko katika hali mbaya, kutokana na matatizo yaliyotokana na ubinafsishaji wa viwanda hivyo.

Mnyika alitoa ushauri huo jana jijini Dar es Salaam,  ambapo alisema waziri huyo mpya katika wizara hiyo, ana wajibu wa kurekebisha matatizo yaliyoko katika sekta za viwanda na biashara ili kunusuru uchumi wa Nchi.

Alisema seta hizo, zina kasoro mbalimbali zilijitokeza wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ambapo  Dk Kigoda alikuwa Waziri katika  Ofisi ya Rais (Mipango na Ubinafsishaji) na kwamba huu ndio wakati wa kurekebisha kasoro hizo.

 “Hatua ya Dk, Abdalah Kigoda kuteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara inapaswa kuwa fursa kwake, kurekebisha makosa ya awali  ikiwa pamoja na ubinafsishaji wa viwanda, kuratibu urekebishaji wa mashirika ya umma na kusimamia kisera utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa,”alisema Mnyika.


Mbunge huyo alisema waziri huyo anapaswa kutanmbua kuwa matatizo ya Kiwanda cha Urafiki ni zaidi ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato mzima wa ubinafsishaji na udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi.

“Kama inavyofahamika, moja ya viwanda vikubwa vya nguo hapa nchini ni kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kilijengwa kutokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka ya China. Pamoja na kuwa muwekezaji wa kiwanda hicho yeye ndie mwenye hisa  nyingi na kwamba anawajibika zaidi katika uendeshaji wa kiwanda na kuangalia  maslahi ya wafanyakazi,” alisema.

Licha ya kuitaka  wizara kunusuru viwanda vya ndani, pia alizitaka  Wizara ya Fedha,  Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali ya Mashirika ya Umma (CHC) na  Wizara ya Kazi na Ajira na Mamlaka kuchukua hatua za kunusuru kiwanda cha Nguo cha Urafiki.

“Nimeamua kuzitaka mamlaka hizo kuchukua hatua, kwa kuzingatia kuwa  Serikali ilifanya ukarabati mkubwa wa mitambo kwa gharama za walipa kodi ambao ni Watanzania,” alisema mbunge huyo.
Mwisho……………..

No comments:

Post a Comment