Saturday, June 30, 2012

Migogoro katika familia ilivyochangia ongezeko la watoto wa mitaani

Hawa ndiyo watoto waliokimbia nyumbani kutokana na migogoro ya familia

TANZANIA imeadhimisha miaka 50 ya uhuru, huku  ikiwa na changamoto kubwa ya ongezeko la watoto wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Ongezeko hilo la watoto hao wanaishi katika mazingira magumu ikiwemo wale wa mitaani inatokana na kukithiri kwa migogoro katika familia pamoja na njaa hali.  

Tumeona mara nyingi wazazi wengi wanapokuwa na migogoro katika familia, wanashindwa kutunza familia zao kikamilifu, ikiwemo kushindwa kuwapa malezi bora watoto wao.

Takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF)  zinasema kuwa, idadi ya watoto wanaoishi mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu inakadiriwa kufikia 120 milioni.

Wakati huo, asilimia  nne ya watoto hao wa mitaani hufanyiwa ukatili baada ya  kuvunjika kwa ndoa za wazazi wao.

Miongoni mwa watoto hao, 30 milioni wako katika bara la Afrika ambapo Tanzania ni moja kati ya nchi hizo yenye changamoto kubwa ya ongezeko la watoto wa mitaani kila kukicha.

Watoto milioni  50 kati ya hao ni yatima kwa sababu mbalimbali ikiwamo  Ukimwi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa eneo la kusini mwa jangwa la Sahara limeripotiwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto wanaofanyishwa kazi ngumu na hatari katika bara la Afrika.

Takwimu  hizo zinaeleza kuwa zaidi ya theluthi moja ya watoto hao wana umri ulio kati ya miaka 5 hadi 14 na wanafanyishwa kazi ngumu.

Kulingana na UNICEF, katika bara hilo la Afrika, maelfu ya watoto wanateswa, kutumiwa vibaya pamoja na kufanyiwa ukatili.

Anasema ni wakati sasa kwa jamii kujikita katika kuimarisha misingi ya familia bora na malezi, kwani hatua hiyo itasaidia kupunguza watoto wa mitaani.

Mbali na takwimu hizo, Utafiti uliofanywa hapa nchini Agosti, mwaka 2009 na shirika  lisilo la kiserikali la Uingereza “Consortium for Street Children” umebaini kuwepo idadi kubwa ya watoto wa mitaani.

Utafiti huo ulifanyika katika miji mikuu saba hapa nchini umebaini sababu mbalimbali zinazochangia kuwepo kwa idadi hiyo huku njaa na ukatili wa majumbani vikiongoza.

Miji hiyo ni Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida na Kilimanjaro na kwamba ulibaini ongezeko kubwa la idadi ya watoto wanaishi mitaani huku jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa kuwa  kitovu cha watoto wanaoishi mitaani.

Mbali na takwimu hizo, imebainika kuwa asilimia 50 ya watoto wanaoishi mitaani  pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu inatokana na ukatili unaofanywa majumbani dhidi ya watoto hao.

Kadhalika asilimia 35 ya watoto hao wanaoishi mitaani inatokana na watoto hao kuzikimbia familia zao  kutokana na njaa pamoja na umasikini uliokithiri katika familia hizo.

Kwa mujibu wa ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani duniani kwa sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 100.

Licha ya kuwapo sheria zinazowalinda watoto juu ya ukatili  lakini inaonekana kuwa sheria hizo bado hazijapewa kipaumbele kama sheria nyingine.

Katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo hufanyika Juni 16 ya kila mwaka, Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya watoto nchini, Tukae Njiku, anasema serikali ina haja ya kuangalia upya tatizo la ongezeko la watoto wanaoishi mitaani kutokana na hali halisi na ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini.

Njiku anasema hivi sasa wizara imeandaa mpango mkakati wa kutokomeza tatizo la watoto wanaoishi mitaani na kuimarisha ushirikiano kati yake na halmashauri  za wilaya  na Manispaa, Miji pamoja na  mashirika yasiyo ya kiserikali katika kukabiliana na tatizo hilo.

Anasema wizara imeamua kubadilishana uzoefu wa jitihada zilizopo kutoka kwa wadau ili kuelewa majukumu na wajibu wa kila mmoja katika kudhibiti tatizo hilo.

Mbali na wizara hiyo kubadilishana  uzoefu, pia imeweka mikakati kwa halmashauri  na jamii ili kupambana na changamoto za kuondoa kero ya ongezeko la watoto wanaoishi mitaani hususan katika miji mikuu ya hapa nchini.

Sanjari na wizara hiyo kuonyesha njia ya kupunguza idadi ya watoto wanaoishi mitaani lakini bado inachangamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa inapunguza idadi hiyo kama sio kuondoa kabisa watoto hao wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Anasema wizara tayari ipo katika mchakato wa kuandaa  kanuni za maadili ya sheria  ya mtoto ya mwaka 2009 ambayo inalenga  kumlinda  mtoto dhidi ya ukatili  na kumpatia fursa ya kumwendeleza.

Njiku anasema kuwa kabla ya kutungwa kwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009, masuala ya mtoto nchini yalikuwa yameainishwa katika sheria ya malezi sura ya 278,sheria ya kuasili mtoto sura ya 335,sheria ya udhibiti wa nyumba za watoto sura ya 61 pamoja na sheria ya watoto na vijana sura ya 13.

Anasema  mbali na kutungwa kwa sheria hiyo, bado  inaonekana kuwa sheria nyingi zinasababisha  ugumu katika uelimishaji na utekelezaji wa masharti kutokana na ugumu uliopo hali ambayo inalazimisha  kuwa na idadi kubwa ya watoto wa mitaani hapa nchini.

Hata hivyo inaonekana kuwa pamoja na sheria hiyo kupitishwa lakini utekelezaji wake ni mdogo ikilinganishwa na jinsi matukio ya watoto yanayotokea.

Anasema  wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wale  wote  watakaobaini kufanya  vitendo  vya ukatili kwa watoto watachukuliwa hatua  kwa mujibu wa sheria hiyo.

“Ifike wakati kwa wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana na serikali kuhamasisha watoto hao juu ya kujenga ufahamu na kusimamia  sheria na haki za watoto ili kupunguza kasi ya kuwepo kwa watoto wa mitaani,” anasema Njiku.

Hata hivyo kama wizara itafanya jitihada ambazo ilizitoa siku ya mtoto wa Afrika basi ni matumaini kuwa ongezeko la watoto wa mitaani litapungua kwa kuwadhibiti watoto hao kuanzia kwenye jamii, Halmashauri hadi Manispaa.

Njiku anasema, ni wazazi  hawana budi kurudi katika misingi ya maadili ili waweze kuwajibika kuwatunza watoto.

Serikali  na jamii kwa ujumla vina wajibu wa  kuongeza juhudi  katika kulinda  maslahi ya watoto kwani ndio taifa la kesho.

No comments:

Post a Comment