Meli STAR GET ya Kampuni ya SEAGULL iliyokuwa na abiria 248 imezama jana eneo la Chumbe
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema
meli ya STAR GET mali ya kampuni ya SEAGULL Transport Company imezama
leo, katika kisiwa cha Chumbe, Zanzibar ilikuwa na abiria 248 wakiwemo
watoto 31 na watalii 10.
Taarifa ya mamlaka hiyo hiyo imesema,
meli hiyo, MV SKY GET iliondoka katika Bandari ya Dar es Salaam leo saa
sita mchana, ikiwa na mabaharia tisa.
Taarifa nyingine (si za
SUMATRA) zinasema sababu ya kupinduka kwa meli hiyo inadhaniwa kuwa ni
kutokana na upepo mkali uliosababisha mawimbi kuipiga nakupindukia
upande mmoja.
Inaelezwa kuwa abiria wengi wameokolewa kutokana na
jitihada mbali mbali kupitia msaada wa boti za Mv Kilimanjaro, Tug ya
Bandari na vyombo vingine. Waliojeruhiwa wanatibiwa katika Hospitali ya
Mnazimmoja.
Kwa mujibu wa SUMATRA meli hiyo imesajiliwa na
Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kwamba, Cheti cha Ubora
kimeanza tarehe 24 Agosti, 2011 na kinamalizika 23 Agosti, 2012.
Imesema, meli hiyo ilikuwa imeruhusiwa kubeba abiria wanaoruhusiwa 300
na tani 26 za mizigo.
“SUMATRA
kupitia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ilipata taarifa kuwa meli
ya MV SKY GET iliyokuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar
ilikuwa inazama katika eneo la karibu na kisiwa cha Chumbe, Zanzibar,
eneo ambalo lipo umbali wa Kilomita za Bahari 13.8 kutoka Bandari ya
Zanzibar” imesema taarifa hiyo.
Kwa
mujibu wa Sumatra, baada ya kupata taarifa hizo, kituo cha MRCC kilitoa
taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya usafiri
wa majini vilivyokuwa karibu na eneo la tukio.
“
Zoezi la uokoaji linaendelea katika eneo la tukio kwa msaada wa vyombo
vifuatavyo: Mv Flying Horse, Mv Kilimanjaro III, Tug Bandari ya
Zanzibar, KMKM, Mv Zanzibar I, Police Patrol Boat, Navy” imesema taarifa
hiyo.
Inaripotiwa kuwa hadi sasa, watu zaidi ya 145 wameokolewa na miili ya maiti 16 imeopolewa.
Waziri
wa Ulinzi Dkt. Emmanuel Nchimbi alisitisha kusoma hotuba ya Wizara yake
kwa kutumia kanuni ya 58 kifungu cha 5 kuomba kutoa hoja iliyokuwa
inaendelea, ili kujadili jambo jingine muhimu.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed
Shein, wa pili kulia) akiwa na Viongozi Wakuu wa Serikali alipofika
katika Ofisi za Shirika la Bandari, Malindi Unguja kupata taarifa sahihi
ya ajali ya kuzama kwa Meli hiyo. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]
Askari Polisi Wanamaji wakiandaa kwenda kwenye ajali hiyo leo katika Bandari ya Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mwinyihaji Makame akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari.
Wananchi mbalimbali wakishuhudia tukio la kuokolewa watu waliozama na meli ya Star Gate.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwa katika Eneo la
Bandari akishuhudia kuletwa kwa majeruhi mbalimbali waliookolewa.
Spika
wa Baraza la Wawakilishi Pandu Amer Kificho pamoja na mawaziri
mbalimbali wakiwa katika eneo la Bandari wakishuhudia kuletwa kwa
majeruhi mbalimbali waliookolewa.
Mmoja wa majeruhi waliookolewa.
Majeruhi wakipatiwa Mablanketi kwa ajili ya kujihifadhi baada ya kuokolewa.
Watalii na raia wa kigeni pia walikuwemo katika meli iliyozama hawa ni baadhi ya waliosalimika
Abiria waliookolewa kutoka katika meli iliozama ya Star Gate katika bahari ya Chumbe Zanzibar
Abiria aliyeokoka kutoka katika meli iliyozama
Abiria
aliyookoka katika Meli iliozama ya Star Gate akifarijiwa na Jamaa zake
Baada ya kuteremka katika Meli iliowaokoa hapo Bandarini
Waziri
wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad akiwa katika hali ya
huzuni Baada ya kushiriki katika uokoaji na kuwaona Majeruhiwaliookolewa
katika Meli iliozama ya Star Gate wakiteremka hapo Bandarini Zanzibar.
Askari
wa Vikosi mbalimbali wakiwa katika kazi ya Uokozi kwa Abiria waliokuwa
katika Meli ya Star Gate ambayo iliozama katika ikiwa imebeba abiria 250
huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar
[Picha: Yussuf Simai - Maelezo]
TAARIFA YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
KUHUSU
MAAFA YA KUZAMA KWA MELI ZANZIBAR
Meli ya Mv. Star Gate imezama karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki hadi muda huu na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa za kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli hiyo ikizama.
“Tulipata taarifa kutoka Boti ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana waliporipoti kuona meli ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri Mwinyihaji.
Waziri huyo alisema Meli hiyo imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin Kusini mwa Kisiwa cha Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya Malindi.
Waziri Mwinyihaji alisema idadi ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6. “Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la tukio kushirikiana na waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.
Alisema maiti zote zitapelekwa viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya ndugu na jamaa kuzitambua maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Katika Bandari ya Malindi mwandishi wetu ameshuhudia maiti kadhaa zikiwemo za watoto zikishushwa, Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa mbalimbali ya nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake amepoteza maisha.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Mawaziri na baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi walikuwepo kutoa msaada unaohitajika.
Katika eneo la pembezoni mwa bandari ya Malindi, makundi ya wananchi yalikuwa yamekusanyika wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.
Vikosi vya ulinzi na usalama, msalaba mwekundu na watoaji wengine wa misaada ya dharura walifika kwa haraka eneo la tukio.
Hadi sasa kazi ya uokoaji inaendelea karibu na Kisiwa cha Yasin ilikozama meli hiyo.
Meli ya Mv. Star Gate inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd ambayo mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.
Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders kuzama katika bahari ya Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea Kisiwani Pemba ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Taarifa zaidi zitatolewa hapo baadaye.
Imetolewa na:
Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzíbar
Julai 18, 2012
Zanzíbar,Tanzania.
Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzíbar
Julai 18, 2012
Zanzíbar,Tanzania.
Baadhi
ya abiria ambayo wameokolewa katika meli inayomilikiwa na Seagull
iliyobiruka katika eneo la bahari karibu na Chumbe (picha via ZanzibarYetu.wordpress.com
Mmoja wa Majeruhi akipata huduma ya kwanza baada ya kuokolewa
Daktari akitowa huduma ya kwanza kwa mmoja wa majeruhi
Majeruhi wa ajali ya Meli wakiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakipata huduma baada ya kuokolewa
Majeruhi wakiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja
Mwokoaji akiwa na mmoja wa maiti wa ajali hiyo
Waokoaji wakiokoa moja ya maiti wakiwa katika boti ya Kilimanjaro.
Majeruhi wakiwa katika mgongo wa boti hiyo wakisubiri kuokolewa
Baadhi ya Abiria wakiwa katika moja ya combo cha kuokolea wakielea baharini wakisubiri kuokolewa.
Boti ya KMKM ikiwa katika zoezi la kuokowa majeruhi.
Helikopta ya Jeshi la Polisi ikiwa eneo la tukio.
Boti iliyozama ni kama hii, ni ni pacha wake.
Boti ya Fly ikiondoka katika bandari ya Zanzibar kueleke kutowa msaada wa uokozi.
Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Hamad Masoud akiwa katika boti ya Kilimanjaro akiwa sehemu ya tukio ilikozama boti.
Tagi la Shirika la Bandari likiwa katika sehemu ya tukio.
No comments:
Post a Comment