Wednesday, August 1, 2012



Katiba ya Nchi si mali ya WanaCCM hivyo isihodhi mjadala wa Katiba - Moyo

 

KATIBA YA NCHI SI MALI YA WANA CCM ASEMA HASSAN NASSOR MOYO MUASISI WA MAPINDUZI NA MUUNGANO WA TANZANIA, ATAKA CCM ISIHODHI MJADALA WA KATIBA.

01/08/2012
Picture: Hassan Nassor Moyo
Mwanasiasa Mkongwe Hassan Nassor Moyo akizungumza na Waandishi wa Habari mbalimbali kuhusiana na Mambo ya Muungano hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Rumaisa Bwawani Zanzibar (picha: ZanzibarYetu.wordpress.com)

Na Abdallah Vuai

Katiba ya nchi sio mali ya Chama cha siasa, ingawaje baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar vyama vingi vya siasa vilifutwa na kutangazwa kuwepo kwa vyama viwili tu yaani ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanganyika, hivyo kufanya katiba kuwa mali ya vyama hivyo.

Ilivyokuwa katiba katika Taifa lolote la kidemokrasia, lenye kuheshimu misingi ya utu ni mali ya wananchi na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya taifa lao.

Aidha, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ya Watanzania wote na kamwe si ya chama tawala cha CCM, makada wake au makamanda wa vita vya ufisadi, hivyo si haki suala la mabadiliko ya katiba ya nchi yakafanywa ni maagizo elekezi ya kufuatwa na wananchi na zaidi wanachama wa CCM.

Kwa sasa CCM haina uhalali sio tu wa kuhodhi katiba ya nchi bali hata kutoa agizo kwa umma kwamba wafuate mtazamo wake katika kutoa maoni juu ya katiba mpya. Natambua kuwepo kwa msimamo wa CCM kuhusu wanachama wake kuwataka wakatoe maoni katika Tume ya Jaji Warioba wasema wanataka Serikali mbili!

Hapa leo ndipo hoja yangu itakapojikita,lakini zaidi nitautizama msimamo huo wa CCM kwa upande wa pili wa shilingi kwamba ikiwa kuna wanachama wasiokubaliana na maoni hayo ya ‘kupewa’ nini tafsiri yake? Lakini pia katika nchi huru yenye kufuata misingi ya haki za binadamu kwa kuzingatia katiba ya nchi, haipendezi kuwalazimisha watu kuacha maoni yao kufuata ya Chama au kikundi fulani.

Msimamo wa CCM kuwashurutisha wanachama wake kwenda kusema wanataka Serikali mbili umewanyang’nya haki ya kimsingi ya uhuru wa kufikiri,lakini pia tunaweza kupata katiba mbovu yenye mawazo yanayolingana na hii naweza kuitafsiri kuwa zile nguvu za

watawaliwa kuwadhibiti watawala zimeondolewa na kuwa kinyume chake watawala kuwadhibiti watawaliwa.

Watu wafahamu kuwa kama kuna nchi ikaanza kutoa maoni na mapendekezo yake kwa wananchi ili wachangie kwa lengo la kufanyia mabadiliko katiba ya nchi, tambua kuwa katiba inayotaka kutungwa au kurekebishwa ni ya watawala.

Katika hili lazima wananchi na hasa Wazanzibari waelewe kwamba katiba ya nchi inapaswa kuwa ni mali yao na tena inayo mahusiano ya moja kwa moja na maisha yao ya kila siku na kwa muktadha huo ni lazima pia mabadiliko yoyote yaanze kutoka kwao.

Akina Nape Nnauye mnaposema mwana CCM atakayekwenda kutoa maoni tofauti na yaliyobatizwa na NEC ya Chama chenu ni kuviza demokrasia na kuwafanya wanachama wenu uwezo wao wa kufikiri mdogo jambo ambalo mimi siliamini hata kwa mtutu wa bunduki.

Dola ya Tanzania inaongozwa na CCM ni jambo la kustajabisha Chama hicho kinapingana na uamuzi wa Serikali yake katika suala zima la katiba mpya, kwamba Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kupata maoni ya wananchi kuhusu jambo hilo, kama CCM haikuwa ikitaka mawazo tofauti wangeiambia Serikali isiunde Tume.

CCM kuwafunga midomo wanachama wake ni sawa na kuwa na kiungo katika mwili kilichopooza ambacho hakiwezi kufanya jambo lolote kimezidiwa hata na mwana sesele anayetiwa betrii akacheza cheza. 


Picture
Tunashukuru Mungu kuwa katika Mkoa wa Kusini Unguja si wanachama wa CCM wala wa vyama vyengine waliofuata maagizo elekezi ya vyama vyao, bali wametoa mitazamo yao na ndio maana kwenye ngome ya CCM Kusini Unguja maoni ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano yameshika kasi.

Kwa maana nyengine wameyapuuza maagizo elekezi ya Chama chao, hivyo CCM na viongozi wake wanapaswa kujithamini upya maana hali ndio hiyo ule wakati wa ‘zidumu fikra za Mwenyekiti’ umeshapita, hakuna mawazo ya kushikiwa.

Mara nyingi CCM haijifunzi kutokana na makosa yake, kama wangekuwa wanajifunza matokeo ya ripoti ya Jaji Nyalali na Jaji Robert Kisanga wasingekuja na maagizo yasiyotekelezeka kwa wanachama wao maana kwa wakati ule asilimia kubwa walitaka mabadiliko katika Muungano, hawakuchangia maoni kama walivyotakiwa na Chama chao.

Sote tunafahamu matokeo ya ripoti ya Jaji Kisanga, Chama tawala na Rais wake kwa wakati huo Benjamin Mkapa walikuwa wakali na kwa sehemu kubwa walichukizwa na taarifa hiyo kwa sababu ilidhihirisha kwamba si wananchi wala Kamati inayokubaliana na matakwa ya Watawala.


Tunaelezwa kwamba ni wananchi laki sita tu ndio waliochangia maoni na katika hao wapo pia waliopinga moja kwa moja maoni ya serikali, na kubakisha idadi ndogo tu ya wananchi wasiozidi laki nne waliokubaliana na maoni ya Serikali.

Wengi hawakwenda kutoa maoni yao na hii inaweza kusababishwa na mambo mengi,lakini kubwa ni kwamba wananchi hawa ni watu wazima wenye akili timamu hawapendi maoni ya kupewa mkononi, kila mtu yuko huru na hilo limethibitishwa na kupewa nguvu kwenye katiba yetu.

Hatutaki kuamini kwamba haki na demokrasia ni maneno tu yanayotumiwa na Chama tawala ili kuwalaza usingizi mnono wananchi huku wakinyimwa haki yao ya msingi ya kushiriki kutoa maoni wanayoyaona yanafaa.

Wazanzibari wakati umefika sasa tukaachana na ushabiki wa vyama vya siasa tukaendelea na juhudi zetu kudai mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano na bila shaka tuungane kufikiria kuhusu mustakbali na hatima ya nchi yetu Zanzibar vyenginevyo, kwa ‘kuiendekeza’CCM itatufikisha ging’ingi.

Hali ya kiuchumi tuliyonayo Zanzibar kwa miaka 48 ni matokeo ya mfumo mbovu wa muundo wa Muungano, sera zake za kiuchumi haziisaidia Zanzibar kuwapeleka mbele katika kuwa na uchumi endelevu na imara, tutaendelea kusambaza bakuli kwa wajomba mwisho watatuchoka.

Kama unalo wazo ambalo unadhani linaweza likaleta manufaa usikae kimya kwa kuhofia tamko la kina Nape, Vyama vya siasa ni vya kupita tu,lakini Zanzibar itaendeela kuwepo, tujiulize viko wapi leo vyama vya siasa kabla ya Mapinduzi?

CCM wasifikiri Wazanzibari wamelala usingizi fofofo, ikiwa wataamini hivyo basi wakae wakijuwa kuwa kioo kimewacheza kizazi cha leo cha Zanzibar sio kile cha mwaka 1964 na kwa kuthibitisha haya tazama maoni yaliyotolewa Mkoa wa Kusini Unguja kuhusu katiba mpya.

Mlalahoi mwenzangu fahamu kwamba unapowasikia viongozi wa CCM, wakihubiri kwamba wametoa mamauzi yale kwa sababu ndivyo wananchi wanavyotaka, kaa ukijuwa wananchi wanaokusudiwa hapo ni vigogo wenziwao, wewe mlalahoi unaeishi Mwakaje, Mikunguni, Fuoni, Darajabovu, Chumbuni huna chako, wewe utapewa wali na pilau, kanga na kikoi na kisha utupwe kwenye mavumbi mpaka baada ya miaka mitano tena ndio ukumbukwe kuja kupewa tena pilau, kanga na kikoi.

Vyama vya siasa kuanza kuwatisha wanachama wake kuwafukuza uanachama ni sawa kuwafanya watumwa ndani ya nchi yao, maana watakuwa si huru kusema yale wanayoyataka, wakitoa maoni tofauti ambayo hayawapendezi Muhafidhina wataanza kutumia rungu la Chama kutisha wanachama.

Kwa tamko la CCM tafsiri yake ni kwamba watu hawana uhuru wala haki ya
kutofautiana mawazo. Yeyote anayetofautiana na tamko hilo anahesabiwa kama muasi,mchochezi, msaliti.

Ni jambo la kusikitisha kuona Tanzania baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika na miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar watu wanakosa uhuru ndani ya nchi huru basi hawezi kuendelea hata kama nchi hiyo ingerundikiwa utajiri wote wa dunia, kama leo mtu anafundishwa au anashurutishwa kutoa maoni yasiyoyake na asiyeyaamini hili ni tatizo kubwa katika demokrasia yetu.

Tukumbuke kuwa nchi nyingi zilizopiga maendeleo watu wake walikuwa na uhuru, watu wasio huru hawawezi kusonga mbele kimaendeleo kila siku tukariri kama kasuku maoni ya watu fulani na ndio maana mipango mingi ya maendeleo haitekelezeki kwa sababu haikupangwa na watu wenyewe, imepangwa na wakubwa Serikalini.

Kwa sasa Wazanzibari tuna vipaumbele vyetu katika katiba na zaidi kuliko yote suala zima la Muungano watu wanataka mabadiliko katika mfumo wa muundo wake, wameuchoka muundo wa sasa ambao hauwaletei faida za kiuchumi.

Hivyo basi, suala la kutoa maoni kuhusu katiba mpya kutekwa nyara na tamko la CCM ni kudhihirisha kuwa madai ya wananchi kwamba CCM, wanaelekea kuwa na nia ya kutokuheshimu matakwa ya wananchi katika kuilea na hatimae kuikuza demokrasia ya kweli Tanzania.

Wengi tunaamini kuwa katiba ndio nguzo ya Taifa na pia ndio sheria kuu ya nchi, kwa sababu hiyo, kigezo cha kwanza cha kuthibitisha kama kweli nchi ina muelekeo wa kidemokrasia ni kuonekana kwa misingi ya demokrasia katika mchakato wa utoaji maoni katika Tume ya Jaji Warioba.

CCM inaelekea kutaka kukumbatia utawala wa kiimla, kwa kuwalazimisha watu kusema wanayotaka wao. Watu wa Tanganyika wanayao katika mabadiliko ya katiba, watu wa Zanzibar pia wana mambo yao ambayo jambo la kwanza kabisa ni Muungano.

Je, wanachama wa CCM watabakia kama watu wa kusadiki kila kitu au watafuata wosia wa Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete aliposema akili za kuambiwa changanya na zako.

Picture
Baadhi ya Waandishi wa Habari mbalimbali waliohudhuria Katika Mkutano wa Mwanasisa Mkongwe Hassan Nassor Moyo akizungumzia mambo ya Muungano hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Rumaisa Bwawani Zanzibar. (picha: ZanzibarYetu.wordpress.com)

Hotuba ya Rais Kikwete ya kuaga Julai na Audio ya majibu ya maswali ya Wanahabari

 
Mwisho kabisa mwa hotuba (kwa maandishi) kuna pleya yenye audio ya maswali ya Wanahabari na majibu ya Rais.

HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2012 


Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kuomba radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba, leo tarehe 01 Agosti, 2012 badala ya jana tarehe 31 Julai, 2012.  Hii ni kwa sababu ya msiba uliotukuta katika familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya marehemu wetu.  Tofauti na miezi iliyopita leo, pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa fursa kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami kujibu.  Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo nitayazungumzia leo.

Ajali ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT

Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012.  Meli hiyo ilikuwa na watu 290, wakiwemo mabaharia 9,abiria watu wazima 250 na watoto 31.  Juhudi za uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo kupatikana.  Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki pamoja na meli na watu binafsi katika uokoaji.  Waokoaji walifanikiwa kuwapata ndugu zetu146 wakiwa hai na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012.  Kwa maana hiyo basi, watu 18 hawajulikani walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai.  Huenda wamezama pamoja na meli au walizama baharini lakini miili yao haikuweza kupatikana.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ile.  Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa waliokolewa, waliojeruhiwa na waliofariki.  Kwa wale ambao walikuwa wenyeji wa Unguja na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa maiti mpaka makwao kwa mazishi.  Kwa wale wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu la kuwazika kule Kama, Kusini Unguja.

Natoa pongezi za pekee kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao ziliwezesha ndugu zetu wengi kusalimika na maiti nyingi kupatikana.

Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali ile kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa yaliyolipata taifa letu miezi 11 iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander.  Katika mkutano maalum wa Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012 kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa maagizo yetu ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV Spice Islander.  Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji umekuwa mzuri kwa upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA, Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili.   Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo Baraza liliagiza wafanye hivyo.   Pamoja na hayo Baraza limetaka ushirikiano huo uzidishwe na kuimarishwa.

Kwa mfano, Baraza limefurahishwa na kupongeza  kitendo cha mamlaka hizo kutumia Dar es Salaam Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora wa meli na huduma za usafirishaji majini.   Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe na hadidu za rejea zinazofanana kwa vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe  na viwango vinavyofanana vya ubora wa meli na huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano.  Bahari ni moja na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya ubora wa meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la hatari.  Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli zilizokwishatumika zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.

Aidha, Baraza limerudia kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa mizigo na abiria.  Mamlaka husika, yaani SUMATRA, ZMA na maofisa wa bandari  wahakikishe kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa unaheshimiwa ipasavyo.  Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo vifanane.

Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo, Baraza la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali yetu kuwa na Coast Guards, yaani kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini.  Aidha, Baraza limetaka hatua za makusudi zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police Marines.  Mwisho, Baraza lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza ajali ile kama ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.

Utafutaji na Uchimbaji Gesi Nchini

Ndugu Wananchi,
Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi asili nchini.  Juhudi za kutafuta mafuta nchini zilianza mwaka 1952 na mwaka 1954 wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha kwanza kule Mafia.  Bahati mbaya kisima hicho hakikuzaa matunda yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta zikafifia kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1960.  Miaka kumi baadae, juhudi hizo zilianza upya na kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa.  Katika miaka ya hivi karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubwa na madogo.

Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 1954, mpaka sasa visima 61 vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi na visima 8vya bahari ya kina kirefu.  Hatujabahatika kupata mafuta lakini tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa baharini na nchi kavu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba ya gesi asili iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9.  Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi kugundulika katika miaka michache ijayo.  Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na hasa gesi baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18. Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010, shughuli za utafutaji sasa zimepamba moto na zimekuwa na mafanikio.  Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea kupatikana.

Fursa za Maendeleo

Ndugu Wananchi;
Kwa kiasi cha gesi asili kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi zaidi kupatikana kunaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani kwa upatikanaji wa gesi asili miaka michache ijayo.  Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya kuweza kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka sasa.

Gesi asili ni rasilimali inayoweza kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia katika kuendeleza kilimo nchini kwa kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei nafuu.  Gesi asili inaweza kutumika kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha na kuwepo ziada ya kuuza nje.  Hivi sasa, katika gridi ya taifa megawati 350za umeme zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500 ifikapo maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili kuwezesha hilo kutimia.  Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam una shabaha hiyo.

Ndugu Wananchi;
Vile vile, gesi asili inaweza kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia mafuta na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji.  Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili kupikia hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni.   Inapunguza gharama za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti.  Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC inatekeleza mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani katika jiji la Dar es Salaam.
Jambo lingine muhimu kuhusu rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata mapato mengi tena ya fedha za kigeni.  Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali yataongezeka sana, hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi.  Kama matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa nchi.  Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo kusaidia kuwaondoa wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao sasa.

Changamoto Muhimu

Ndugu Wananchi;
Pamoja na ukweli kwamba kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya kujiletea maendeleo, zipo pia changamoto zake. Hatuna budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili gesi iweze kunufaisha ipasavyo nchi yetu na watu wake.  Changamoto zipo nyingi lakini kubwa zipo za namna tatu.

Changamoto ya kwanza ni ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli zinazofanywa na makampuni ya mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo yanayostahili.  Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu wazalendo wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia, jiofizikia, uhasibu, ukaguzi na sheria.  Tusipojenga uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya kudhulumiwa na kupata hasara.  Pengine ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa ajili hiyo kama tulivyofanya kwa mafanikio kwa upande wa dhahabu.

Changamoto ya pili ni ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika na soko la ajira la sekta ya gesi.  Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka nje na hivyo kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.

Ndugu Wananchi,
Kwa changamoto hizi mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu katika shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu.  Kwanza kabisa lazima tuboreshe elimu ya sayansi na hisabati katika shule zetu za msingi na sekondari.  Katika vyuo vya ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma zinazohitajika na tasnia ya gesi na mafuta.  Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo vikuu nako wafundishe wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa gesi na mafuta, uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na gesi, uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi na mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo ya Chemical and Environmental Lab for Oil and Gas na fani ya Exploration and Production Software Technologykatika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia Septemba mwaka huu. Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es Salaam  pia wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha, VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao wanafundisha masomo yahusuyo gesi.  Wizara ya Nishati na Madini itawadhamini wanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA Mtwara.

Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati na Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati ya 40-50 kati ya sasa na mwaka 2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum Geoscience, Petroleum Geophysics, Petroleum Geochemistry, Petroleum Engineering, Petroleum Modeling, Oil and Gas economics, Oil and Gas Accounting and Auditing na Oil and gas Legal Regimes and Contract Negotiations.  Kwa upande wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za mafunzo ili tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana wetu wachangamkie fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari kuitumikia nchi yetu kwa bidii.

Kujenga Uwezo Wetu wa Kutumia Mapato ya Gesi

Ndugu Wananchi,
Changamoto nyingine kubwa sana ni ile ya kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi yanatumika vizuri na kwa manufaa ya taifa na watu wake.  Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa ajili hiyo.  Si vyema tukangojea mpaka hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia na kutumia mapato yatokanayo na gesi.  Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu watakuwa wameanza kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo utakaowanyima fursa ya kuliibia taifa.

Jambo hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo mifano hai ya nchi zenye rasilimali nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na wananchi wake hawanufaiki sawia.  Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana lakini manufaa  kwa nchi na watu wake ni madogo au hayapo kabisa. Wanaonufaika ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi wa shughuli zihusuzo rasilimali hizo.  Na, hata sisi tunaweza kujikuta katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.

Ndugu Wananchi;
Zipo nchi duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa mapato ya rasilimali za mafuta na gesi na kuleta baraka na neema kwa taifa na watu wake.  Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia vizuri mapato yake kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa watu.  Matokeo yake ni watu wa nchi hizo kuishi maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya kupatikana kwa rasilimali hizo.  Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi.

 Tumeamua kujifunza kutoka nchi za wenzetu waliofanikiwa ili na sisi tunufaike.  Na sisi tunajiandaa kutengemeza Sera ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali yatokanayo na gesi zitakazotoa majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na gesi hiyo.  Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa na baadae hutolewa kwa utaratibu maalum.  

Tunataka tujifunze kutoka kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili tunufaike.

Ndugu Wananchi;
Mambo hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi.  Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na mashirika ya maendeleo ya kimataifa, nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na kushirikiana kwa mambo mawili.  Kwanza kwa kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu watakaosaidia kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na biashara ya gesi asili nchini.  Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi na uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya  kutengeneza mifumo bora ya kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu waliofanikiwa. 

Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri na nchi zote na mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao.  Baada ya muda si mrefu kazi itaanza.

Mgomo wa Walimu

Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu na la mwisho ni mgomo wa walimu.  Pengine ni mapema kusema kwa vile kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo. Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu.  Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo mbalimbali.  Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo.  Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.  Haitakuwa sawa.  Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.

Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu:  Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi.  Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao.  Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.

Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote nchini kheri na baraka tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo mema katika mfungo huu. Mkumbuke pia kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.   

Baada ya maneno hayo, naomba sasa niishie hapo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. 

Sasa nipo tayari kujibu maswali ya Wahariri kama yapo. Ndugu Wahariri mliopo hapa, karibuni.   

MATUKIO KUTOKA BUNGENI DODOMA LEO


Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe akielekea ndani ya ukumbo wa Bunge mjini Dodoma Aug,1,2012 kwaajili ya kusoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa Fedha,2012-2012 (Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO).
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais- Asiye na Wizara Maalumu Prof, Mark Mwandosya akitoa shukurani Aug,1,2012 kwa Serikali na Wananchi waliomuombea wakati akiwa mgojwa hadi kupata nafuu na kuweza kuhudhuria tena katika vikao vya Bunge ,mjini Dodoma. (Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO).
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki akijibu hoja mbalimbali  Bungeni leo kuhusu wizara yake, (Picha na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO).
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (kulia) akitoa maelezo binafsi kwa waandishi  wa habari Aug. 1,2012 kuhusu tuhuma za rushwa dhidi yake hususan kuelekea katika kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati. Pichani mwengine ni  Prof. Koyela Kahigi (CHADEMA). Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO,






No comments:

Post a Comment