Thursday, August 2, 2012


JK:Aahidi Kifuta Jasho Cha Ng'ombe 1500 Kwa Wananchi Wa Wilaya Tatu Za Mkoa Wa Arusha

SERIKALI itakuwa inagawa ng’ombe 1500 kila mwezi kwa wananchi wa wilaya tatu za Mkoa wa Arusha kama kifuta jasho cha kupoteza kiasi cha karibu mifugo 800,000 iliyopotea kutokana na ukame na athari zake mwaka 2008/2009.

Ahadi hiyo imetolewa leo, Alhamisi, Agosti 2, 2012 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipozindua Mradi wa Serikali wa Uwezeshaji Mifugo kwa waliopotelewa mifugo yote katika Wilaya ya Monduli kwenye sherehe iliyofanyika Makuyuni wilayani humo.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Arusha wakiwemo wakuu wa wilaya na wabunge wa mkoa huo, Rais Kikwete amegawa ng’ombe 500 kwa kundi la kwanza la wananchi ikiwa ni mitamba minne na dume moja la kisasa kwa kaya 16 za mwanzo.

Uzinduzi huo ni wa pili kufanywa na Rais Kikwete chini ya Mradi huo wa kwanza wa aina yake kubuniwa na Serikali katika historia na wenye thamani ya sh. Bilioni 12.9.

Februari 19, mwaka huu, Rais Kikwete alizindua Mradi kama huo katika Wilaya ya Loliondo kwenye sherehe zilizofanyika mjini Loliondo. Kesho Agosti 3, 2012 Rais Kikwete anatarajiwa kuendelea na zoezi hilo katika mji wa Loliondo 

DK KIGODA AITAKA TBS KUFANYA UKAGUZI WA BIDHAA KUTOKA NJE YA NCHI


WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amelitaka Shirika la Viwango (TBS), kuhakikisha linafanya ukaguzi wa bidhaa kutoka nje kabla hazijaingizwa nchini ili kuepukana na tabia nchi hii kugeuzwa dampo la bidhaa hafifu.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana, wakati alipokuwa akizindua Ofisi ndogo ya shirika hilo, inayoshughulika na ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Dk Kigoda alisema iwapo shirika hilo litafanikiwa kudhibiti uingizwaji wa bidhaa hafifu nchini anaamini kelele zote zinazopigwa kuwa wao ndio chanzo cha uingizwaji wa biadhaa hizo zitakwisha.
“Nawaagiza TBS kupitia madukani na sokoni ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa ubora wa bidhaa na zile bidhaa mtakazokuta ni hafifu, zitoweni na kuziharibu na hao wafanyabishara watozwe faini za kuharibu bidhaa zao”alisema Dk Kigoda.
Alibainisha kuwa Wizara yake inatarajia kupata taarifa juu ya utekelezaji wa maagizo hayo kwa vipindi vya kila robo mwaka ili kujua utaratibu wa utekelezaji.
Akifafanua madhumuni ya wizara ni kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kama vile Mamlaka ya Mapato (TRA) Baraza   la Mazingira ,Mamlaka ya Chakula na Madawa (TFDA), Mkemia Mkuu wa  serikali, pamoja na  Tume ya Ushindani  ili kuhakikisha bidhaa za nje zinapimwa maridhawa.
“Ili shehena za bidhaa hafifu zizibitiwe kuingia sokoni na kurudishwa zilikotoka” kwa mujibu Dk Kigoda.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi  ya shirika hilo, Oliver Mhaiki   alitabanaisha kwamba uzinduzi wa ofisi hiyo ni muendelezo wa jitihada za shirika kusogeza huduma kwa wateja.
Vile vile alifafanua kuwa TBS  imeshapanua wigo kwa kufungua ofisi katika maeneo mbalimbali kama vile Sirari, Holili, Horohoro, Bandari ya Tanga sanjari na Namanga mkoani Arusha, kwa lengo la kuwasogezea huduma wadau na kuwapunguzia adha katiaka shughuli zao za kibiashara.
 

RAMBIRAMBI MSIBA WA MSAFIRI MKEREMI


 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa kimataifa Msafiri Mkeremi kilichotokea leo alfajiri (Agosti 2 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Licha ya kuwa mwamuzi, Mkeremi aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) sasa TFF kwa vipindi viwili tofauti. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT).
 
Vilevile aliwahi kuwa mkufunzi wa waamuzi, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Pwani.
 
Kwa upande wa vyama vya mpira wa miguu aliwahi kuwa kiongozi katika mikoa ya Tabora, Pwani na wilayani Mpanda katika Mkoa wa Rukwa.
 
Msiba wa Mkeremi uko nyumbani kwake Urambo, na kwa mujibu wa mtoto wake Masoud Mkeremi, atazikwa Jumamosi kwenye makaburi ya Msafa yaliyoko wilayani Urambo.
 
TFF inatoa pole kwa familia na kuitaka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
 
Marehemu aliyekuwa akisumbuliwa na presha na ugonjwa wa kisukari ameacha wajane wawili na watoto 12.  Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina
 

HakiElimu waishauri Serikali, CWT kuhusu mgomo wa Walimu

Na Joachim Mushi, Thehabari.com
 
TAASISI ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.
Mkurugenzi huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya  watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza mgogoro huo.
“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu  na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi,” alisema Missokia.
Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
 

Waziri Mkuu Mizengo Pinda Katika Maonyesho Ya NaneNane

 Waziri mkuu, Mizengo Pinda akikagua mkungu wa ndizi katika maonyesho ya wakulima Nanenane Mjini Morogoro Agosti Mosi 2012. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua mafuta ya mawese yaliyokamuliwa katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Ruvu wakati alipotembelea Banda la Jeshi hilo kwenye  maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agosti Mosi, 2012. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama mzinga wa asili wa nyuki wadogo wakati alipotembelea banda la Magereza kwenye maonyesho ya Wakulima Nanenane Mjini Morogo Agosti Mosi, 2012. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 
 

No comments:

Post a Comment