Thursday, January 3, 2013
JESHI la Polisi mkoani Iringa limewafukuza kazi askari Polisi wake wawili G 402 D/C Denis Beatus na F 3277 D/C Karume Farija Kunga baada ya kushiriki katika jaribio la kupokea rushwa.
Askari hao wanadaiwa kupokea rushwa hiyo kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa pembe za ndovu waliokuwa wakishikiliwa na jeshi hilo tangu Desemba 10, mwaka jana kwa lengo la kupatiwa dhamana.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliwakamata askari hao pamoja na Katibu wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali mkoani hapa na kisha kupandishwa kizimbani Desemba 31 mwaka jana kwa tuhuma za kuomba rushwa ya sh milioni sita ili wawasaidie watuhumiwa wa pembe za ndovu.
Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Iringa, Consolatha Singano kujibu kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni sita kutoka kwa washtakiwa watatu wa nyara za serikali, Abdul Abdallah, Patrick Raymond na Hamsi Solomoni.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Imani Mitume, alidai jalada la kesi hiyo namba 306 ya mwaka 2012 lina mashitaka saba.
Alidai kuwa askari namba G 402 D/C Denis Beatus (32) na Joshua Mkwama (37) na Katibu wa Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Iringa, Joshua Mkama, wanakabiliwa na shitaka la kwanza la kuomba rushwa ya sh milioni sita.
Aliongeza kuwa Beatus anakabiliwa na shitaka la pili la kupokea rushwa hapo Desemba 12 mwaka huu, kutoka kwa Diska Gadama ili kuwasaidia ndugu zake wapate dhamana katika kesi ya kukutwa na nyaraka za serikali kinyume cha sheria.
Mwendesha Mashitaka huyo, alidai kuwa Mkama, anakabiliwa na shtaka la tatu la kupokea rushwa ya sh milioni tatu kutoka kwa Joshua Mkwama katika ofisi ya mwanasheria Desemba 16 mwaka huu.
Kwamba askari namba F 3277 D/C Karume Kunga (32), anakabiliwa na shitaka la nne la kupokea rushwa ya sh. laki tano kutoka kwa Beatus.
Diska Kashinde Gandama mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam ambaye ni ndugu wa washitakiwa watatu wanaokabiliwa na kesi ya kukutwa na nyaraka za serikali, anakabiliwa na shitaka la tano la kutoa rushwa kwa Beatus katika kituo kikuu cha mabasi mkoa wa Iringa.
Shitaka la sita linamkabili Beatus na Gandama ambao wanadaiwa kutoa rushwa ya sh 3,000,000 na kumpa Mkama ili kuwasaidia Patrick na wenzake katika kesi inayowakabili.
Katika shitaka la saba, ilidaiwa kuwa Beatus alimkabidhi Karume Farijala rushwa ya sh laki tano ili kuhujumu kesi dhidi ya nyaraka za serikali inayowakabili watu watatu.
Washtakiwa wote walikana mashitaka na mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Januari 15 mwaka 2013.
Washtakiwa wa pembe za ndovu walikamatwa saa 7:45 katika kijiji cha Mtandika, Tarafa ya Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo, Iringa mnamo Desemba 10 mwaka jana wakiwa na pembe za ndovu 78 zilizokadiliwa kuwa na thamani ya sh 934,830,000.
via gazeti la Tanzania Daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment