Sunday, November 24, 2013

SOMA

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
Zitto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu aliingia katika malumbano na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa na Lema kuwa anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho kutoka mashirika mbalimbali nchini. 
 
1. Utangulizi
i. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 ­ 22 Novemba 2013, Kamati  Kuu  ya  CHADEMA,  pamoja  na mambo  mengine,  iliazimia  kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa  katika  mkutano  na  waandishi  wa  habari  siku  ya  Ijumaa  tarehe 22 Novemba  2013,  ilielezwa  kwamba  sababu  za  kuvuliwa  uongozi  mimi  na  Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati  Kuu  ni  tuhuma  lukuki  ambazo  si  mara  yangu  ya  kwanza  kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.

Nitazianisha  tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.

ii. Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba
 mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi  nilivyo.  Ningependa  chama  hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama  changu na  ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.

2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu

Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi  ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba  mimi  ni  mbinafsi  na  kwamba  ninapokea rushwa  ili  kukihujumu  chama changu.  Nitazianisha  tuhuma  kwa  kifupi  na  kuzijibu  kama  ambavyo  nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.

i)  Tuhuma  kwamba  sikushiriki  kumpigia  kampeni  mgombea  wetu  wa  urais  katika uchaguzi wa mwaka 2010.   Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.

● Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.

● Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.

● Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii)  Tuhuma  kwamba  katika  Mkoa  wa  Kigoma  nilishindwa  kuwapigia  kampeni wagombea  wetu  kiasi  kwamba  peke  yangu  ndiye  niliyeshinda  katika uchaguzi huo.

Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.

iii)  Tuhuma  kwamba  nilishiriki  kuwashawishi  wagombea  wetu  katika  baadhi  ya majimbo  kujitoa  katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite  bila  kupingwa  kwa  njia  ya  rushwa.  Majimbo  yanayotajwa  ni pamoja  na Sumbawanga,  Musoma  Vijijini  na  Singida  Mjini. Kama  nilivyokwisha  kueleza  katika vikao  mbalimbali  vya  chama  jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma  hizi  wamewahi  kutoa  ushahidi  kwamba  nilifanya  jambo hili. Nipo  tayari  kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.

iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni  kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada  ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa  na  operesheni  kubwa  moja  katika  mikoa  ya  kusini  ya  Mtwara  na  Lindi.

Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.

v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):  Katika  jambo  hili  ninatuhumiwa  kwamba  mimi  kama  Naibu  Katibu nilipaswa  kuwasiliana  kwanza  na  viongozi  wa  chama  'kuwatonya'  ili  wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili  kuadhibiwa  vikali  kwa  kuwa  katika  taarifa  yangu  nilikuwa  na  nia  mbaya na chama  chetu.  Maelezo  yangu  niliyoyatoa  na  ambayo  ningependa  kuyakariri  hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:

● Utawala  bora  hautaki  mimi  kutumia  nafasi  yangu  ya  uenyekiti  wa  PAC  kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha

● Napenda  kusisitiza  kwamba  hakuna  chama  ambacho  kimewahi  kukaguliwa  na Mdhibiti  na  Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).  Natambua  kwamba  mahesabu  ya chama  changu  yamekuwa  yakikaguliwa  na  wakaguzi  wa  nje  kwa  utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao

Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi  mengine  yasiyofaa  katika  fedha  za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu  ya  mwaka  2010­2015.  Mtakumbuka  kwamba  hivi  karibuni  Mheshimiwa  Lema amenishutumu  kwamba  kukataa  kwangu  kuchukua  posho  ni  unafiki  kwa  sababu ninapokea posho  kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Sipokei  posho  yeyote  ya  vikao  (sitting allowance)  ndani  na  nje  ya  Bunge tangu mwaka  2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.

● Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu  ni  swala  la  kimisingi  zaidi.  Katika  Wilaya  yangu  vifo  vya  kina  mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama  chetu  kuliweka  swala  la kupunguza  matumizi  ya  Serikali  katika  Ilani,  na kuondoa  posho  za  wabunge,  ambao  tayari  wanapokea  mishahara  mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.

● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.

3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe

Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa  kuwa  umechomolewa  kutoka  makao  makuu  ya  CHADEMA.  Jambo  hili  pia lilijadiliwa katika  kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba  waraka  huu  haukuandaliwa  wala  kusambazwa  na  makao  makuu.  Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:

i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama  chetu.  Bahati  mbaya  hadi  leo  hakuna  hata  mmoja  ambaye amekwishachukuliwa  hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.

ii. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za  kisheria  ili  kuhakikisha  kwamba  wote  waliohusika  kutengeneza  hekaya  ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

4. Hitimisho

a) Ninatambua  kwamba  kuna  watu  walitegemea  leo  ningejibu  mapigo  na ningewazodoa  watu  kwa  majina  kama  ilivyo  kawaida  katika  siasa  za  Tanzania.

Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.

Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia  suala  hili  katika  harakati  zao  za  kudhoofisha  mapambano  ya demokrasia  na  uthabiti  wa  siasa  za  ushindani  nchini  mwetu.  Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue  kwamba  mimi  bado  ni  mwanachama  mwaminifu  wa  chama  hiki  na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.

b) Naomba  wanachama  waelewe  kwamba  mimi  kama  binadamu  ninaumia ninapopigwa.  Tuhuma  ninazorushiwa  ni  kubwa  na  zinanikwaza.  Tuache  siasa  za uzushi  ili  tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.

c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri  nimeyafanya.  Lakini  kuna  maeneo  nilipojikwaa  na  yapo  makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.

d) Kinachoendelea  ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano  baina  ya  wapenda  demokrasia  dhidi  ya  wahafidhina,  waumini  wa uwajibikaji  dhidi  ya wabadhirifu  na  wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.  Hii  ni  changamoto  kubwa  ndani  ya  chama  chetu  inayohitaji  uongozi shupavu  kuikabili.  Nitasimama  daima  upande  wa  demokrasia. Kama  alivyopata kunena  mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.

Taarifa ya Dk Kitila Mkumbo juu ya kuvuliwa nafasi za mamlaka ndani ya CHADEMA

1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA. Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi ujao ndani ya chama.

2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa hoja za watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani ya chama hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa kukubali ombi langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na kueleza kuwa
nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida hadi hapo chama kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.

3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe) tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:

a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama chetu.

b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini. Chama hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo. Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’.

Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho nilijisababishia matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho chama kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa.

c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa imani niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo demokrasia, na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.

d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani. Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi mkali sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda uteuzi wa kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha Democrat mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka maalumu wa siri ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne tu bila yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya Hillary Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha urais. Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.

e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yeyote kuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari.

f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua nafasi yangu moja kwa moja. Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa nayo. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.

4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.

5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe. Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za ukomunisti katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika nchi. Zilikuwa ni njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.

6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania.

Mungu ibariki Tanzania.

Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.

Taarifa rasmi kwa umma kutoka CHADEMA, Novemba 2013

UTANGULIZI

Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 20 Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013 imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na 
tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu, yaani Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa. Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na athari ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na Chama chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande vipande na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Uchunguzi wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika  waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama ‘MM’ au ‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye waraka anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.

Kwa mujibu wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri kwamba MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye mwenyewe Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata kata kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba yote yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye ‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.

Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua pasua CHADEMA na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa njia za kidemokrasia na za kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na kukiua. Ndio maana watunzi wa waraka huu wamesema kwenye waraka wao: “Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio maana hata lugha iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati Kuu inaamini mkakati wenye malengo halali ya kufanya mabadiliko ndani ya Chama kwa njia halali za kikatiba usingependekeza kwamba: “Vikao vyetu na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe) vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita kiasi ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba kama mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio kukiteka nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza utaratibu ufuatao wa utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye atakayekuwa anawasiliana na tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu). Tumepanga kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa.”

Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana chana Katiba ya Chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya Chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba.

1. Wakati ibara ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama ambazo ni sehemu ya Katiba ya Chama chetu ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa CHADEMA asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii”, wanaMtandao wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa wanaendekeza siasa za udini kwa kusema yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu tunayemtaka’, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe: “Kwa kuwa ni Mwislamu, hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.”

2. Wakati ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila kiongozi wa CHADEMA “… kuwa mkweli na muwazi wakati wote … na aachane na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) …”, wanaMtandao wa Ushindi wameeleza kwenye waraka wao kwamba mipango yao ya utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 ‘itafanyika kwa usiri mkubwa.’

3. Wakati ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama inamtaka “kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”, wanaMtandao wa Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa (ambaye wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni ‘Mpinzani wetu’) kuwa “… hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na dharau nyingi anazozionyesha pale anapokutana na viongozi wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii…. Hii imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi za chini hivi sasa na kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.”

4. Wakati ibara ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka “kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote zilizotolewa na wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu hazijawahi kutolewa na yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao chochote halali cha Chama cha ngazi yoyote.

5. Wakati ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji inaeleza kwamba “itakuwa marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu Chama, kiongozi au mwanachama yeyote wa Chama …”, Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa, matusi mengi na udhalilishaji mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na wanachama kwa ujumla. Hivyo, kwa mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa na wanaMtandao hawa kuwa ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia shaka’, mwenye ‘elimu ya magumashi’, ‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye akili ndogo’, n.k.

Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Hakuna chama au taasisi yoyote duniani inayoweza kunyamazia mkakati wa aina hii dhidi yake na viongozi wake wakuu na ikadumu au kubaki salama. Chama au taasisi yoyote inayoendekeza vitendo vya aina hii miongoni mwa viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa wanachama wake wa kawaida inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi wake wa juu wamekaa kimya kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na kashfa nyingi sana dhidi yao binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi makubwa sana dhidi yao. Chama chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake wamevumilia yote haya sio kwa sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu ulitokana na haja ya kuwapa wanaMtandao wa Ushindi fursa ya kugundua hatari ya siasa zao na kuwapa muda wa kujirekebisha na kujirudi.

Kama ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa Chama chetu na viongozi wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha uvumilivu wa Chama chetu, viongozi wake na wanachama wake kama wanavyowakilishwa na Kamati Kuu ya Chama chetu. Hivyo basi, katika kikao chake tajwa, Kamati Kuu ya Chama chetu, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeazimia yafuatayo kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi:
(a) Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya Chama;

(b) Kwamba timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya Makao Makuu ya Chama na wajumbe wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili kumtambua mtu anayeitwa M2 na ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa Makao Makuu ya Chama ili hatua stahiki na za haraka zichukuliwe dhidi yake, pamoja na watu wengine wote watakaobainika kuhusika na mpango huu wa uhaini dhidi ya Chama chetu;

(c) Kwamba Kamati ya Chama ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate effect;

(d) Kwamba viongozi waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati zenye tuhuma dhidi yao haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe kwenye Chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea kama inavyotakiwa na ibara ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama;

(e) Kwamba mara baada ya utekelezaji wa azimio (d), Kamati Kuu ikutane kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua nyingine zitakazofuata;
(f) Kwamba waraka wa wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi uwekwe hadharani na usambazwe kwa vyombo vya habari vya aina zote ili wananchi wa Tanzania, wanachama na viongozi wa Chama chetu na dunia nzima kwa ujumla iweze kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na uhalali wa maamuzi haya ya Kamati Kuu.

Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya Mkakati wao wa kukiteka nyara Chama na kukiangamiza kujulikana mbele ya Kamati Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia Chama, viongozi wake wakuu na wanachama wake kwa ujumla; na kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa nyadhifa kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na kwa kuzingatia uelewa wao wa Katiba, Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu wao katika safu za juu za uongozi wa Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa kauli moja kuridhia maombi hayo ya kujiuzulu. Kufanya hivyo ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu wajiondoe kwenye uongozi wa Chama wakiwa na heshima wasizostahili hata kidogo.

Chama chetu ni tumaini pekee la Watanzania wote wanaotaka mabadiliko ya kweli na ya kimsingi katika mfumo wa kiutawala, kiuchumi na kijamii wa nchi yetu. Hii ndiyo sababu kubwa na ya pekee iliyosababisha vita kubwa na chafu inayopigwa dhidi ya Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo kuu ni kuwachafua viongozi wakuu, kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya wanachama, viongozi wake na hivyo kukichafua Chama mbele ya macho ya Watanzania. Chama chetu kikishachafuka kwa mtindo huu, matumaini ya Watanzania wanaotaka mabadiliko yatakufa. Vita hii kubwa haijaanza jana, na haitaisha kesho. Kama ambavyo tumekabiliana nayo na kuishinda siku za nyuma, vivyo hivyo tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda. Kama Chama chetu kilivyoibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika mapambano ya siku za nyuma, vivyo hivyo Chama chetu kitaibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika awamu hii ya mapambano.

Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu wasife moyo, bali waendelee kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa tama, kila mmoja wetu aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale wanaotaka kuleta majanga katika Chama chetu na kwa Taifa letu.
FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB),                                                            WILBROD PETER SLAA
MWENYEKITI,  TAIFA                                                                                         KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment