Thursday, July 19, 2012



Maiti wa ajali ya MV Skagit watambuliwa; Wasiotambuliwa wamezikwa na Serikali


Baadhi ya miili ya maiti ya waliookolewa kutoka katika MV Skagit iliyozama hapo jana, wakitambuliwa na ndugu zao katika Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar, na kuruhusiwa kuichukuwa kwa ajili ya taratibu za mazishi. 
Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Lenhardt Alfonso wakatikati akionekana na huzuni Baada ya kuziona Maiti zilizookolewa katika Meli iliozama hapo jana katika Bahari ya Chumbe Zanzibar.Balozi alifika katika Viwanja vya Maisara ili kuona namna shughuli za kushughulikia maiti zinavyoendelea. 
Mama alietambulika kwa Jina la Bitatu Uyelo ambae amenusurika na kupoteza mtoto wake wa miezi tisa katika ajali ya MV Skagit. 


Waziri wa Mambo ya ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emanuel Nchimbi alifika katika eneo lililohifadhiwa Maiti wa ajali ya MV Skagit ili kutambuliwa na ndugu zao na kupata maelezo kwa Daktari Kiongozi (hayupo pichani) katika Viwanja Vya Maisara Zanzibar. 
Baadhi ya Maiti waliookolewa kutoka katika MV Skagit na kukosa watu wake, wakipelekwa kuzikwa na Serikali katika Eneo la Kama lililotayarishwa makusudi kwa ajili hiyo. 
----
[Picha na maelezo: Yussuf Simai - Maelezo via ZanziNews blog]

 
 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji mmoja wa walionusurika katika ajali ya meli jana huko Chumbwe wakati Rais na Mama Salma Kikwete walipowatembelea kuwafariji na kuwapa pole katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja leo Julai 19, 2012.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakitembelea Uwanja wa Maisara, Zanzibar, ambako ndiko miili ya marehemu huletwa kwa utambuzi baada ya kuokolewa kwenye eneo la ajali leo Julai 19, 2012.


Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete wakimsikiliza mmoja wa walionusurika katika ajali ya meli jana Bw Kitwana Makama Haji ambaye kalazwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja leo Julai 19, 2012 




Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete wakimpa pole Bi Salome Abeli, mmoja wa walionusurika katika ajali hiyo ya meli. Yeye ni mfanyakazi wa Tanzania Automic Energy Commission akitokea Arusha kwenda Pemba Kikazi leo Julai 19, 2012. 






PICHA: IKULU


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji Khamis, jinsi ulivyandaliwa utaratibu wa kuwahifadhi marehemu watakaokosa kutambuliwa na ndugu zao, wakati Makamu alipofika kwenye Viwanja vya Maisara mjini Zanzibar, leo Julai 19, 2012, kuangalia shughuli za uokoaji na utambuzi wa marehemu. Kushoto ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsikiliza mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya Meli ya Skagit, Kitwana Makame Ali (24) mkazi wa Unguja, wakati alipotembelea katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, leo Julai 19, 2012 kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo baada ya kuokolewa katika ajali hiyo iliyotokea jana eneo la Kisiwa cha Chumbe. Kulia ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan. 

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsikiliza mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya Meli ya Skagit, Masembe Enos (32), mkazi wa jijini Mwanza aliyekuwa akisafiri na mkewe ambaye mpaka sasa hajapatikana.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na mgonjwa aliyenusulika katika ajali ya Meli ya Skagit, Hamisa Akida (45) mkazi wa Ununio mjini Bagamoyo, wakati alipotembelea katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, leo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza  mmoja kati ya vijana walionusulika katika ajali ya Meli ya Skagit, Stephano Lufyagila (22), mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na vijana wawili, Hans Manoni (kulia) na Nsunga Joseph, waliokuwa wakisafiri na wenzao wawili ambao wamefariki katika ajali hiyo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsalimia Salome Abeid Mwambaga (33) mkazi wa jijini Arusha, mfanyakazi wa Kampuni ya Atomic Enegy Commissioner, aliyekuwa akisafiri kuelekea Pemba kikazi ambaye pia amepoteza vifaa vya kazi na Document zake zote muhimu katika ajali hiyo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kumpa pole kuhusu ajali ya Meli ya Skagit mali ya Kampuni ya seagull, iliyotokea jana eneo la Kisiwa cha Chumbe.

 Wananchi wakiwa wamepanga foleni kuelekea kutambua miili ya marehemu katika Viwanja vya Maisara leo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujionea shughuli hizo katika viwanja vya Maisara mjini Unguja leo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akijumjuika na wananchi katika moja ya familia iliyopotelewa na ndugu katika ajali hiyo, mjini Zanzibar leo mchana.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na mgonjwa aliyenusulika katika ajali ya Meli ya Skagit, Hamisa Akida (45) mkazi wa Ununio mjini Bagamoyo. 

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar leo Julai 19, 2012 kwa ajili ya kumpa pole kuhusu ajali ya Meli ya Skiget mali ya Kampuni ya seagull, iliyotokea jana eneo la Kisiwa cha Chumbe.
 
 

Orodha ya majina ya abiria wa MV Skagit itabandikwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dar es Salaam

19/07/2012
 
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imebandika orodha ya majina ya wasafiri 340 waliokuwa katika meli ya Mv Skagit huku wananchi wakitakiwa kukuhakiki kama ndugu zao walikuwemo.

Aidha, Polisi jijini Dar es Salaam inamshikilia Meneja wa meli hiyo, Omar Hassan Mkamnhongt (50) mkazi wa Magomeni ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Seagul Transport Tawi la Dar es Salaam inayomiliki meli hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck amesema Polisi Kanda Maalumu inafanya uchunguzi wa ajali hiyo, wakishirikiana na wadau mbalimbali kusaidia utambuzi wa waliokufa, majeruhi wa Tanzania bara na wa Zanzibar pamoja na watalii kutoka nje.

Akizungumza na baadhi ya wanandugu waliofika ofisini kwake, Sadiki amesema, licha ya kubandika orodha hiyo, ofisi yake haina uhakika na idadi hiyo kwani huenda walikuwepo zaidi ya hao. Alisema orodha ya majina hayo itabandikwa katika ofisi yake na kwamba kila mwanandugu anayehitaji kufahamu zaidi anatakiwa kufika na kutambua majina hayo.

Alisema ofisi yake pia inajaribu kuzungumza na wamiliki wa meli au boti wasaidie wanandugu wanaotaka kwenda Zanzibar kutambua ndugu zao waliofikwa na mauti kwenye ajali hiyo, “Wapo wanandugu hapa ambao wana uwezo na wanataka kwenda Zanzibar ili kuwatambua ndugu zao, lakini wameshindwa kwenda kutokana na meli nyingine kusitisha safari hivyo hao tunakwenda nao bandarini sasa hivi (jana) ili kuwasaidia waweze kufanikisha safari yao,” alisema na kuongeza: “Kwa wale ambao hawawezi kwenda leo (jana) tutahakikisha tunafanya utaratibu ili kesho waweze kwenda kwa ajili ya kutambua maiti.

Kuhusu usalama wa meli hiyo, Sadiki alisema kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi wa meli hiyo, inaonesha kwamba ilikaguliwa Agosti 24 mwaka jana na kwamba ilikuwa inamalizika muda wake Agosti 23, mwaka huu, “Si kweli kwamba meli ilikuwa haijafanyiwa uchunguzi… polisi wanafuatilia zaidi… na kuanzia leo (jana) tunatengeneza fomu maalumu yenye jina la aliyepotea na anayetaka kwenda Zanzibar kutambua maiti ambapo ataandikisha jina lake kwa Edward Mbanga aliyeko katika ofisi za Mkuu wa Mkoa,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema juzi walituma kundi kubwa la watu kwa ajili ya kusaidia shughuli ya kuokoa.

Kova aliwataka ndugu na jamaa wa watu wanaohofiwa kufa katika meli hiyo, waorodheshe majina ya ndugu zao, nguo walizokuwa wamevalia ili kikosi chake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) walioko eneo la ajali, wasaidie kuwatambua.
  

"Kuna watu 11 wakiwamo waandishi 2 wa habari, nitawatwanga kweupe" - Membe

19/07/2012
 
Juzi alipozungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV na kuongozwa na Mtangazaji wa ITV, Selaman Semeyu, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alizungumzia pamoja na mambo mengine, fedha za mkopo, Dola za Marekani milioni 20 zilizokuwa zimetolewa na Serikali ya Libya enzi za utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hayati Muamar Gaddafi.

Pia aligusia upotevu wa Sh bilioni tatu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Akizungumzia fedha hizo, Membe alisema baada ya Serikali ya Libya kuikopesha Serikali ya Tanzania kiasi hicho cha fedha, baadaye Serikali za nchi hizo mbili zilikutana na kukubaliana fedha hizo zikopeshwe kwa kampuni yoyote itakayozihitaji.

“Baadaye Serikali ya Libya na Tanzania zilikutana na kukubaliana fedha hizo zikopeshwe kwa kampuni yoyote itakayotaka kukopa izikope na makubaliano haya yako kwenye maandishi. Baadaye ikaja kampuni moja ya Meize kwa ajili ya kujenga kiwanda cha saruji kule Lindi na wakati wa kampeni tukawaahidi wananchi wa Lindi kwamba kiwanda hicho kitajengwa. Wakati tunaahidi hivyo, kumbe Kampuni ya Mohamed Enterprises ilikuwa inashirikiana na ofisa mmoja wa ubalozi wa Libya apate fedha hizo na hapo ukawa ugomvi.

“Pamoja na hayo, mimi nilisimamia kuhakikisha kiwanda hicho cha saruji kinajengwa Lindi kama sehemu ya kumbukumbu yangu. Lakini baadaye wananume wakabadilisha lugha, wakasema nimewapa marafiki zangu, jamani fedha hizi ni makubalino ya nchi mbili na mimi ni ‘share holder’.

“Sasa nakwambia fedha hizi ziko TIB, nendeni kwa meneja wa TIB mumuulize, huu ujinga gani huu unaozungumzwa, kwanza hata hizo Dola milioni 20 hazitoshi kujenga kiwanda bali zinatakiwa Dola milioni 60.

“Sasa nataka niwaambie wananchi wa Lindi kwamba kiwanda cha saruji kitajengwa Lindi, hivi vituko vinavyotokea nitavigonga vyote na ipo siku nitawaanika wote, lazima watu hao wajue kwamba ukikaa juu ya nyoka, ipo siku atakugonga tu. Hili nawaachia Watanzania waamue lakini kuna watu 11 wakiwamo waandishi wawili wa habari, nitawatwanga kweupe, nyie suala la urais 2015 subirini tu nitawaanika peupe bungeni tena kwa majina,” alisema Waziri Membe.

Suala la urais 2015

Alipoulizwa kama atagombea urais mwaka 2015, alishindwa kuweka wazi msimamo wake kwa kile alichosema kuwa hajaoteshwa juu ya nafasi hiyo.

“Ole wao nioteshwe, ipo siku nitaoteshwa, najua nchi hii ina watu wanaoivuruga na hawataki kuona mafanikio, ukisema unataka kujivua gamba utaona wana uwezo wa kuchonga uongo, hao wanatumia vyombo vya habari kuchonga uongo. “Kwa mfano, unawakaribisha vijana kama wa Chadema nyumbani kwako unawapa chakula baadaye wanageuza mambo, we waache tu.

“Siku moja nitawatoa kwenye magazeti kila mmoja dozi yake, nitakuja kuwatandika kila mmoja na kinachoniudhi ni kwamba hao watu wako ‘smart’ wana fedha na wanataka kutawala hata kama hawana madaraka. Ukiona mtu anaanza kudharau wakati hana madaraka, ujue hapo kuna tatizo. “Jambo jingine ni kwamba ukianza kuona katika jamii kila tatizo inalaumiwa Serikali, ujue kuna tatizo, ujue hapa kazi ipo.

Uchaguzi ndani ya CCM

Kuhusu uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema chama hicho kina nafasi ya kujiimarisha kupitia uchaguzi huo. Alisema ana hamu ya kufika mwaka 2015 ashuhudie uchaguzi mkuu utakavyokuwa.

“Nina hamu ya kufika mwaka 2015 nione akina nani watarudi maana kuna wabunge wengine ni mahodari wa kuzungumza bungeni lakini majimboni hawaendi. “Utakuta mbunge mwingine anasema haungi mkono bajeti, lakini baada ya siku mbili anamuomba Waziri aliyepinga bajeti yake kwamba naomba fedha za kupeleka jimboni kwangu. “Upinzani siyo kukataa bajeti, huwezi kukataa bajeti yangu halafu kesho unakuja kuniomba fedha upeleke jimboni kwako,” alisema.

Alitaka Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naye awe anaulizwa maswali ya papo kwa papo kupima uwezo wake katika utendaji.

Maoni ya wabunge

Wakizungumza juu ya kauli za waziri huyo, baadhi ya wabunge wameonyesha kutoridhishwa kutokana na nafasi aliyonayo katika Serikali.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alisema kitendo cha Membe kusema kuna watu 11 wanaiyumbisha Serikali, hakitakiwi kufumbiwa macho kwa kuwa kinagusa mamilioni ya Watanzania, “Huyu Membe aache maneno, hivi majuzi alisema kuna watu anawafahamu wanahusika na mauzo ya rada, sasa anakuja na suala jingine la watu 11 wanaoyumbisha nchi. “Kama kweli anawajua kwa nini asiwataje, yaani wananchi wanataabika halafu yeye anatwambia atawataja, mimi simuelewi, mwambieni awataje,” alisema Mpina.

Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (CHADEMA), alisema Membe anatafuta umaarufu wa siasa kwa kuwa ana kitu anachokitaka, “Huyu tumemzoea, alisema hivi karibuni kwamba anawajua wahusika wa rushwa ya rada na hadi sasa hawajawataja, sasa unafikiri anataka nini. “Kama kweli hao watu wapo kwa nini asiwataje, atutajie majina, lakini kama anadhani kuna watu kama akina Lowassa wanataka kumkwamisha asigombee urais mwaka 2015, anajidanganya kwa sababu yeye hawezi kupambana na Lowassa, huyo ni mtu mdogo kwa Lowassa,” alisema Wenje.

Naye Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alionyesha kutoridhishwa na kauli ya Membe na kusema kuwa hakumuelewa baada ya kutotaja majina ya watu hao 11.

“Mimi nilimuona akizingumza na nilipomsikia hivyo, nikashindwa kumuelewa kwa sababu kama alichokuwa akikisema hakiendani na madaraka yake. “Sasa kama kweli anawajua watu hao 11 kwa nini asiwataje, atutajie kuwafanya wananchi waendelee kuiamini Serikali yao,” alisema Azzan.

Rais mmoja mstaafu wa Zanzibar atajwa kuhusika na usajili wa Meli za Iran

 
Wakati uchunguzi wa kimataifa ungali ukiendelea, gazeti la Raia Mwema limethibitishiwa kuwa Rais mstaafu aliyepata kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na mmoja wa kigogo wa juu wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wanahusika.

Mtandao huo wa kiongozi huyo mstaafu ambaye anazo ndoto za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mwenzake ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wamefanya mpango huo na aliyepata kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia amepata kuwa mbunge wa moja ya majimbo ya uchaguzi mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, tayari vyombo vya kimataifa vinaelekea kukamilisha uchunguzi wake na kwamba, majina ya wahusika hao yatawasilishwa serikalini kwa hatua zaidi.

Kwa ushirikiano maalumu, viongozi hao wanadaiwa kufanikisha meli za Iran kusajiliwa na kisha kupeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kukwepa vikwazo vya kimataifa vilivyoweka kupitia Umoja wa Mataifa (UN).

Vigogo hao wanadaiwa kufanikisha mpango wao kupitia kwa kampuni ya Philtex ya Dubai, inayodaiwa kusajili meli za mafuta za Iran ili kupeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kukwepa vikwazo vya kiuchumi iliyowekewa nchi ya Iran.

Katika toleo lake namba 248, gazeti hili liliripoti kuwapo kwa taarifa kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa zikibainisha kuwa, baadhi ya viongozi Zanzibar wamekuwa na maslahi katika masuala ya usajili wa meli hizo za kimataifa jijini Dubai.

Katika habari hiyo kwenye gazeti hili, mwandishi wetu alinukuu moja ya chanzo chetu cha habari akisema; “Unajua kuna hali ya kuzidiana ujanja, awali huku Zanzibar walikataa SUMATRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Maji na Nchi Kavu) kufanya shughuli zake na wakaunda Wakala wa Meli Zanzibar (ZMA) lakini wakala huyu akatoa zabuni ya kusajili meli kwa kampuni iliyoko Dubai (Philtex),”

“Baadhi ya viongozi hapa Zanzibar hawakujua ujanja uliopangwa na wenzao, ujanja wa kuikataa SUMATRA Zanzibar na kuanzisha ZMA lakini pia ujanja wa kutoa zabuni kwa kampuni ya Philtex ya Dubai. Sasa hivi ndiyo wanashituka kwamba wapo wenzao wanaodaiwa kuhusishwa na kampuni hiyo,” kilieleza chanzo chetu cha habari kutoka Serikali ya Zanzibar.

Ya TANESCO: Akaunti ya kigogo ya Bil. 1/- yazuiwa; Hujuma; Wabunge wanahusishwa


 
SIKU chache baada ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO), William Mhando na wenzake: Robert Shemhilu, Lusekelo Kassanga na Haruna Mattambo, akaunti ya mmoja wa vigogo wa shirika hilo ngazi ya menejimenti iliyoko katika moja ya benki nchini imezuiwa na vyombo vya dola nchini, Raia Mwema, limeelezwa.

Akaunti ya kigogo huyo (jina la benki na la mwenye akaunti yanahifadhiwa ili kutoharibu uchunguzi unaoendelea) imekutwa na fedha zaidi ya shilingi bilioni moja na sasa inadaiwa kuzuiwa kwa baraka za mamlaka za juu.

Vyanzo kadhaa vya habari vimeeleza ya kuwa kigogo huyo amekutwa na mabilioni hayo ya fedha huku chanzo cha mapato hayo yasiyolingana na kipato chake kama mtumishi wa umma kikiwa ni utata.

Hata hivyo, wakati uchunguzi huo wa awali unaofanywa na vyombo vya dola nchini ukiwa unaendelea, kwa upande mwingine kumebainika kuwapo na kampeni kali za kuuokoa uongozi wa TANESCO unaochunguzwa kwa sasa, juhudi ambazo zimekuwa zikihusisha hata Kamati za Bunge.

Kamati za Bunge ambazo baadhi ya wajumbe wake wanahusishwa katika ‘kuokoa’ jahazi la uongozi wa TANESCO uliosimamishwa ni pamoja na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo sasa wanatajwa kuanza kumwandama Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi pamoja na Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Naibu wake, George Simbachawene, wanaotajwa kuwa na msimamo mkali dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe na ubadhirifu ndani ya TANESCO.

Mgawo feki wa umeme
Hujuma kwa mtambo wa Kinyerezi
Wabunge watajwa

Tume ya Katiba yatoa taarifa ya kusitisha mikutano ya kukusanya maoni kwa siku tatu


 
Alhamisi, Julai 19, 2012

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea jana, Jumatano, tarehe 18,  Julai  2012 katika eneo la Chumbe, Zanzibar.

Kutokana na msiba huu mkubwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa Taarifa kwa Wananchi kuwa imesitisha Mikutano ya kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba. Mikutano iliyositishwa ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia leo, Alhamisi, Julai 19, 2012 hadi Jumamosi, Julai 21, 2012 katika maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara.

Zoezi la kukusanya Maoni litaendelea kuanzia  Jumapili tarehe 22, Julai, 2012.  Ratiba ya Mikutano katika maeneo yaliyositishwa itatolewa baadaye.

Tume ya Mabadilikio ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa mabadiliko haya hayahusu mikutano ya kukusanya maoni inayoendelea kufanyika katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani, Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera na Manyara.  Tume inawaomba wananchi wa Mikoa hii kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao.

Mwisho, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatoa pole kwa wafiwa, majeruhi na wote walioguswa na ajali hii na tunamuomba Mwenye Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na majeruhi wote wapone kwa haraka.

Imetolewa na:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P. 1681,
DAR ES SALAAM,
Simu: 2137833,
Simu ya Mkononi: 0757 500800


 
 


No comments:

Post a Comment