SERIKALI MKOANI IRINGA YASAINI KATABA NA JAPANI KUIKARABATI HOSP[ITALI YA TOSAMAGANGA
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akisoma
taarifa fupi ya mkoa kwa balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada
|
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akimkabidhi
kitabu cha profile ya Mkoa wa Iringa Balozi wa Japan
nchini Tanzania
|
Balozi wa Japan
nchini Tanzania Masaki Okada (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma.
|
Serikali ya Japan imeahidi
kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
sekta mbalimbali hasa katika sekta ya afya na kilimo.
Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa
Japan nchini Tanzania Bw.Masaki Okada alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya
Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Balozi Okada amesema kuwa Serikali
yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania
katika kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya
nchi mbili hizo. Amesema kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania
wanategemea kilimo, ni lazima kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na
kilimo hicho kama shughuli yao
kuu ya kiuchumi. Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya
kilimo nchili ili kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa
nchi ya Japan inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.
Aidha, amezipongeza juhudi za
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo
wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.
Awali katika salamu za Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za Serikali ya Japan
katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni juhudi za kupongezwa sana. Amesema kupitia
misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza kupata ufadhili
katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na umwagiliaji.
Akiongelea maambukizi ya virusi
vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kujibu wa utafiti
wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani asilimia 16 ya maambukizi,
kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha maambukizi kitaifa. Amesema
kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi za pamoja kati ya Tanzania na
Japan katika kuendeleza mapambano hayo. Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali
ya Japan za kuisaidia Tanzania
katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha
afya ya mama na familia katika mkoa wa
Iringa.
Balozi wa Japan nchini Tanzania yupo
mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya
Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza ubora
wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.
MAKAMPUNI 10 KUSAMBAZA PEMBEJEO ZA KILIMO WILAYA YA IRINGA
Kampuni za mbolea zaidi ya 10
zimejitokeza kuhudumia wakulima katika Wilaya ya Iringa kwa ajili ya kusambaza
vocha za pembejeo za kilimo kwa mwaka 2012/2013 na 2013/2014.
Akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa utoaji wa pembejeo zenye ruzuku kwa msimu wa kilimo wa mwaka
2011/2012 na maandalizi ya kilimo msimu wa mwaka 2012/2013 katika kikao cha
kamati ya pembejeo cha mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa
Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa
imepokea utaratibu mpya kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa
usambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa mahindi na
mpunga kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013.
Amesema kuwa utaratibu wa kutumia
vocha utaendelea ila mawakala watakaosambaza pembejeo hizo kwa wakulima
wanufaika na kampuni ya pembejeo ndiyo itasambaza pembejeo hizo badala ya
kamati ya pembejeo ya wilaya kama ilivyokuwa
awali.
Amesema lengo la kampuni za
pembejeo kupewa jukumu la kuteua mawakala ni kuhakikisha pembejeo zenye ubora
zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka. Amesema kuwa kazi ya kamati ya
pembejeo ya wilaya itakuwa ni kusimamia na kufuatilia utaratibu mzima wa
pembejeo katika mchakato wote.
Lucy amesema jumla ya kampuni 13
za mbolea na mbegu zimejitokeza kuhudumia wakulima wa Wilaya ya Iringa. Amesema
makampuni hayo yameteua mawakala wawakilishi saba na mawakala wasaidizi 46.
Akiongelea uhamasishaji wa matumizi ya mbolea ya minjingu mazao pamoja na
utaratibu wa usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kipindi
cha mwaka 2012/2013 na 2013/2014 umefanyika katika vijiji vya Nyabula,
Lupembelwasenga, Usengelindeti, Makombe, Kihanga, Ng’enza, Magulilwa na
Tagamenda. Uhamasishaji huo unaendelea sambamba na usambazaji wa
vocha za pembejeo.
Wakati
huohuo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea mgao wa pembejeo zenye ruzuku
kwa mwaka 2012/2013 zenye thamani ya shilingi 1,828,654,000. Akielezea aina ya
pembejeo hizo, Afisa Kilimo, mifugo na ushirika amesema kuwa mbolea ya kupandia
vocha (22,000), mbolea ya kukuzia (22,000), mbegu ya mahindi (chotara)
(5,409),mbegu ya mahindi mchanganyiko (9,309), mbegu ya mpunga (7,282).
Lucy
ameyataja mafanikio yaliyotokana na mfumo wa vocha kuwa ni upatikanaji wa
pembejeo katika ngazi ya kijiji umefikiwa ambapo wakulima wanaweza kununua
pembejeo katika maeneo ya vijiji vyao. Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni
ongezeko la uzalishaji kutoka gumia 3-5 za mahindi hadi kufikia wastani wa
gunia 12-22 kwa ekari, kwa zao la mpunga ongezeko kutoka gunia 8-10 hadi
kufikia wastani wa gunia 16-25. Aidha,
idadi ya wakulima wanaolima kitaalamu imeongezeka na matumizi ya pembejeo kwa
wakulima yameongezeka.
Akifungua
kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amekiaarifu kikao
hicho kuwa msimu wa kilimo umefika na kuwa mvua zimeanza kunyesha katika baadhi
ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi na wakulima wameanza kupanda. Aidha, aliwataka
wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima katika kuwafundisha na kuwaelekeza
mbinu bora za kilimo.
No comments:
Post a Comment